Guardian Angel afunguka kuhusu uhusiano na watoto wakubwa wa mkewe Esther Musila

Guardian Angel amefunguka kuhusu uhusiano wake mzuri na watoto wake watatu wa kambo.

Muhtasari

•Guardian Angel alisema kwamba anahusiana vyema sana na watoto wote wa mke wake Esther Musila; Gilda Naibei, Glenn Naibei, na Kim.

•Bi Esther Musila alifichua kwamba watoto wake waliingiana vyema sana na mumewe huyo wa miaka 35 tangu mwanzo.

Guardian Angel na bintiye wa Kambo Gilda
Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amefunguka kuhusu uhusiano wake mzuri na watoto wake watatu wa kambo.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na blogu ya hapa nchini, mwanamuziki huyo alisema kwamba anahusiana vyema sana na watoto wote wa mke wake Esther Musila; Gilda Naibei, Glenn Naibei, na Kim.

“Wao ni watu wakubwa. Tuko na uhusiano mzuri, uhusiano mzuri sana,” Guardian Angel alisema.

Kwa upande wake, Bi Esther Musila alifichua kwamba watoto wake waliingiana vyema sana na mumewe huyo wa miaka 35 tangu mwanzo

Aidha, alifichua kuwa .alipoanza kuchumbiana na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili, watoto wake walibaini kwa urahisi kwani kulikuwa na mabadiliko makubwa katika tabia zake.

“Siku moja niliwaambia nachumbiana na mtu huyu. Unajua watoto tu, mimi nikiwa mzazi wao pekee, kulikuwa na dhana kwamba mama amepata mtu, tutaachwaje peke yetu? Lakini Guardian alikuja maishani mwao kwa kishindo. Tangu siku ya kwanza nilipomtambulisha kwao, walikuwa na maelewano mazuri,” alisema.

Huku akiwajibu wakosoaji wa mahusiano yao, Guardian Angel alisema kuwa hajutii kamwe kuchumbiana na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 53.

Alibainisha kuwa wapo wanaume wengi waliooa wanawake wenye umri mdogo kuliko wao, kama ilivyo kawaida katika jamii,  lakini ndoa zikashindwa kudumu.

“Ahadi yangu kwa mke wangu inapita zaidi ya umri. Inaenda zaidi ya maoni ya watu kwa sababu ukiingia kwa hicho kitanda ni wewe na mke wako, hamna jamaa wa maoni. Kwa kuongea na kuongea mitandaoni,” alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 alisema kwamba tangu mwanzo, hakuwahi kujali watu wangesema nini kuhusu uhusiano wake na mama huyo wa watoto watatu wakubwa.