"Esther bado ni wako!" Akothee akiri mapenzi yake mazito kwa Nelly Oaks

Akothee alimsherehekea kimahaba mpenzi na meneja wake Nelson Oyogi almaarufu Nelly Oaks.

Muhtasari

•Akothee alichukua fursa ya kusherehekea mwanaume huyo mwenye miraba minne na kukiri mapenzi yake kwake.

•"Wewe ni valentine wangu mwaka mzima. Oooh NDIO NAMPENDA. Mtu bora wa mwaka 💪 @nellyoaks,” Akothee alisema.

Akothee na aliyekuwa mpenzi wake Nelly Oaks
Akothee na aliyekuwa mpenzi wake Nelly Oaks
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya, Esther Akoth almaarufu Akothee mnamo Jumatano alimsherehekea kimahaba mpenzi na meneja wake Nelson Oyogi almaarufu Nelly Oaks.

Ikiwa ni Siku ya Wapendanao, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alichukua fursa ya kumsherehekea mwanaume huyo mwenye miraba minne na kukiri mapenzi yake kwake.

Alitumia lugha yake ya asili ya Kijaluo na Kiingereza kueleza ni kwa nini Nelly Oaks ni wa pekee sana kwake na kujigamba kumhusu.

Osiepna maromona @nellyoaks eeh wuora ichoka kaka agakni . Kuwa sawa lichni. Kata thoo kata angima pod Esther Mari , Ruoth oriti Wuora,” Akothee aliandika.

Kumaanisha: “Rafiki yangu ambaye huwepo kwa ajili yangu..@nellyoaks, ooh mpenzi umenibeba jinsi ninavyokuwa mgumu kushughulika naye. Na hujali hata. Hata nikiwa nimekufa au ni hai,  Esta bado ni wako.. Mungu akulinde mpenzi!”

Aliongeza, "Wewe ni valentine wangu mwaka mzima. Oooh NDIO NAMPENDA. Mtu bora wa mwaka 💪 @nellyoaks.

Mama huyo wa watoto watano aliendelea kuwaonya watumizi wa mitandao dhidi ya kutoa maoni mabaya chini ya ujumbe wake mzuri kwa Nelly Oaks

Akothee na Nelly Oaks wanaonekana kurudiana baada ya ndoa ya mwimbaji huyo na Denis ‘Omosh’ Schweizer kuvunjika katikati ya mwaka jana.

Bw Nelly Oaks, ambaye jina lake halisi ni Nelson Oyugi ni meneja rasmi wa Akothee na pia anaaminika kuwa mpenzi wake.

Mara nyingi, wawili hao mara wameonekana wakishiriki nyakati nzuri za kimapenzi pamoja hadharani na mara nyingi katika siku za nyuma, Akothee amekuwa akidokeza kuhusu uhusiano kati yao.

Takriban miezi iliyopita, mwanamuziki huyo alionekana kuthibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na meneja wake wa muda mrefu Nelly Oaks katika kipindi cha moja kwa moja cha hivi majuzi kwenye mtandao wa TikTok.

Katika kipindi hicho ambacho alikuwa akiwahutubia mashabiki wake Nelly Oaks akimwandalia chakula maalum jikoni, Akothee alisikika akimwita meneja huyo wake ‘babe’ mara kadhaa, jina ambalo hutumika sana sana  wapenzi.

Nelly Oaks pia alisikika akimtaja Akothee kama mtu maalum kwake huku wawili hao wakishiriki matukio ya kimapenzi kwenye kamera.

“Hiki ni chakula cha jioni maalum kwa mtu maalum kama wewe. Ni surprise,” Nelly Oaks alisikika akimwambia mwanamuziki huyo.

Wakati wa kipindi hicho, Akothee kwa hasira aliwasuta wanawake wote waliokiri mapenzi yao kwa meneja huyo wake akidokeza kuwa hapatikani kwao.

Wakati baadhi ya mashabiki walipotaka kujua iwapo Nelly Oaks ana mchumba, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alionekana kuthibitisha kuwa yeye ndiye anashikilia nafasi hiyo.

“Ati kama Nelly ako na mtu?! Kwani mimi mawe? Mimi mawe? Ama mimi ni mti? Unauliza kama Nelly ako na mtu, kwani mimi ni mawe? Ama kijiti? Usinipimie pumzi. Maisha ni ya kwangu nayaendesha vile nataka,” alisema.

Mama huyo wa watoto watano pia alikataa ombi la nambari ya simu ya Nelly Oaks huku akifichua kwamba hata ana uwezo wa kufungua na kutumia simu yake.

“Kweli nikupatie namba ya Nelly? unadhani mimi nimetosheka? Mimi sijarudi soko, mimi ndiye soko, sigawani na mtu,” Akothee alisema.

Nelly Oaks pia aliweka wazi kuwa hapatikani kwa mwanamke mwingine.