Lupita Nyong’o ajivinjari na mpenziwe mpya miezi baada ya kumtema Selema Masekela

Lupita anaonekana kujitosa kwenye dimbwi nzito la mahaba na muigizaji mwenzake kutoka Canada, Joshua Jackson.

Muhtasari

•Wawili hao walionekana wakiwa wameshikana mikono kimahaba wakitembea kando ya ufuo wa Puerto Vallarta, Mexico.

•Lupita na Jackson walihusishwa kimapenzi kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2023 baada ya wawili hao kutengana na wenzi wao. 

Lupita Nyong'o na mpenziwe Joshua Jackson
Image: HISANI

Miezi michache tu baada ya kuthibitisha kuvunjika kwa mahusiano yake na mtangazaji wa masuala ya spoti Selema Masekela, mugizaji mashuhuri wa Kenya na Canada Lupita Nyong'o anaonekana kujitosa kwenye dimbwi la mahaba na muigizaji mwenzake Joshua Jackson kutoka Canada.

Ripoti za uhusiano wa wawili hao zimekithiri katika muda wa saa chache zilizopita baada ya picha nzuri za waigizaji hao kuibuka kwenye mitandao ya kijamii.

Picha ambazo zilionekana na Radio Jambo zinamuonyesha Lupita na mzungu huyo mwenye umri wa miaka 45 wakiwa wameshikana mikono kimahaba wakitembea kando ya ufuo wa Puerto Vallarta, Mexico ambapo binti huyo wa gavana Anyang’ Nyong’o alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 41. Wawili hao wote walikuwa wamevalia mavazi mepesi ya kuogelea.

Waigizaji hao mashuhuri pia walionekana wakikimbia baharini pamoja na pia karibu wakibusiana katika picha zinazosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Lupita na Jackson walihusishwa kimapenzi kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2023 baada ya wawili hao kutengana na wenzi wao. Joshua aliachana na mkewe Jodie Turner-Smith na Nyong'o akatengana na aliyekuwa mpenzi wake kutoka Selema Masekela.

Lupita Nyong’o alimaliza uhusiano wake na mpenzi wake Selema Masekela mnamo Oktoba 2023 baada ya kuchumbiana kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Lupita ambaye alionekana kuhuzunika alitoa tangazo la kutengana na Masekela kupitia mitandao yake ya kijamii akisema "ni muhimu kwangu kushiriki ukweli wa kibinafsi na kujitenga hadharani na mtu ambaye siwezi kumwamini tena,".

Wapenzi hao wa zamani walitengana takriban mwaka mmoja baada ya kuweka hadharani uhusiano wao.

Lupita alitangaza kutengana kupitia mtandao wake wa kijamii mnamo Oktoba 19, 2023. Wawili hao walitangaza uhusiano wao hadharani mnamo Desemba 2022.

Wakati huo, mwigizaji wa Black Panther alitumia mitandao yake ya kijamii kumpigia debe Selema Masekela - kama ufichuzi kuwa wako kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Lupita alikuwa akichumbiana na Selema Masekela mwenye umri wa miaka 51 akiwa na miaka 39.