"Ita polisi" Akothee afoka baada ya mzazi mwenzake mzungu kumuonya asipike omena, akaidi maagizo

Licha ya wanawe Akothee kulalamika kuhusu harufu ya Omena, walifurahia chakula hicho na hata kuweka zaidi.

Muhtasari

•Jumamosi, Akothee alionyesha video yake jikoni akipika ugali na omena ambapo alifichua kwamba alikuwa ameonywa dhidi yake.

•Akothee alibainisha kuwa alikuwa ameagizwa apike mayai badala ya omena, ila akakaidi akilalamika kuwa wamekula mayai sana.

Baba Ayoo na Akothee
Baba Ayoo na Akothee
Image: INSTAGRAM/AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee alikaidi agizo la baba mtoto wake wa mwisho Baba Oyoo aliyemtaka asipike omena nyumbani kwake.

Mama huyo wa watoto watano kwa sasa yuko nchini Ufaransa kuwatembelea wanawe wawili vijana Prince Ojwang (Alphonse) na Prince Oyoo (Dominic) wanaoishi na Baba Oyoo.

Siku ya Jumamosi, alionyesha video yake jikoni akipika ugali na omena ambapo alifichua kwamba alikuwa ameonywa dhidi yake.

“Naambiwa nisipike omena itanuka kwa nyumba. Omena nitapika. Nilibeba mzigo wangu kutoka Kenya, Omena ndo hiyo,” Akothee alisema kwenye video hiyo huku akionyesha omeni aliyokuwa akipika kwenye sufuria.

Aliendelea kulalamika dhidi ya mzazi mwenzake mzungu na mwanawe Oyoo ambao walilalamikia harufu ya samaki hao wadogo aliokuwa akipika.

“Baba Oyoo piga simu polisi. Ati Oyoo anafunga mapua, nyumba inanuka. Mnafikiri mtanitesa hapa Ulaya, ng’o. Ata Royco ndio hii,” alisema huku akionyesha kontena ya Royco aliyokuwa amebeba kutoka Kenya.

Akaendelea, “Nitapika omena, kisha nitapika ugali na kula. Kisha nitaenda kujifungia chumbani. Nitawacha omena ikinuka hapo kwa jikoni na nimeenda. Ni mambo baby mama.”

Akothee alibainisha kuwa alikuwa ameagizwa apike mayai badala ya omena, ila akakaidi akilalamika kwamba wamekula mayai sana kule.

Akiwa jikoni, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alimwalika mwanawe mdogo Oyoo kwa maswali kabla ya mvulana huyo kulalamika kuhusu moshi ndani ya chumba hicho. Akothee alionekana akiimba na wanawe wawili jikoni na kuwaonyesha baadhi ya miondoko ya densi.

Licha ya kulalamika kuhusu harufu hiyo, Akothee aliwawekea wanawe  ugali na omena na mdogo Oyoo hata akaomba kupewa ugali zaidi.

“Si Jaduong’ alisema watoto wake hawatakula omena. Saa hii wamebeba ugali kubwa na omena wameenda kukua. Baba yake hayuko ameenda ghorofani amesema huku kunanuka na kupiga kelele,” Akothee alisema.

Mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa si rahisi kuishi na wanaume weupe na hata kuwataka wasichana wanaowataka wamtafute ushauri.