Kitendo cha Samidoh kujitokeza kumsapoti bintiye wa kambo chamsisimua Karen Nyamu

Samidoh alionyesha upendo kwa msichana huyo kwa kujitokeza kwenye hafla yake wakati mama yake akiwa Marekani.

Muhtasari

•Seneta Nyamu alitoa shukrani baada ya mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kujitokeza katika hafla ya bintiye Ijumaa.

•"Support system, asante kwa kuwa hapo siku kuu ya mtoto wangu nikiwa mbali," seneta Nyamu alisema.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alitoa shukrani za dhati baada ya mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kujitokeza katika hafla ya bintiye siku ya Ijumaa.

Katika picha zilizoshirikiwa na mwanasiasa huyo, Samidoh alionekana akiwa amemkumbatia binti mzaliwa wa kwanza wa seneta Nyamu, Teana wakati wa iliyoonekana kuwa hafla ya talanta ya shule.

Picha zingine zilimuonyesha msichana huyo mwenye umri wa miaka tisa pamoja na wanafunzi wengine jukwaani huku hadhira, ambayo huenda Samidoh alikuwa sehemu yake ikitazama.

"Support system, asante kwa kuwa hapo siku kuu ya mtoto wangu nikiwa mbali," seneta Nyamu ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani aliandika chini ya picha alizochapisha kwenye mtandao wa Facebook.

Picha hizo zilionyesha uhusiano mzuri ambao mwimbaji Samidoh anao na mtoto wa kwanza wa mwanasiasa huyo, ambaye alizaa akiwa kwenye uhusiano wake wa awali na mcheza santuri DJ Saint Kevin.

Mwishoni mwa mwaka jana, Bi Nyamu alifunguka kuhusu suala la malezi ya watoto wake na kufichua uhusiano mzuri kati ya binti yake Teana na baba zake wawili.

Katika mahojiano kwenye chaneli ya YouTube ya Convo, mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka tisa anawatambua Samidoh (mpenzi wa sasa wa Karen Nyamu) na DJ Saint Kevin (mzazi mwenzake Karen Nyamu) kama baba zake.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alisema Teana huwaita wanaume wote wawili hao ‘baba’ na hata kufanya nao mazungumzo mara kwa mara.

"Huwa anawaita baba wote wawili 'dad'. Na huwa ninamwambia "una bahati sana kuwa na baba wawili," Karen Nyamu alisema.

Aliongeza, “Huwa anapiga simu kwa mmoja anamwambia “Nataka hiki, hiki na hiki” alafu anapigia huyu mwingine anamwambia, “Nataka hiki na hiki."

Wakili huyo pia alifunguka kuhusu uhusiano wake na binti yake akifichua kuwa kwa kawaida huwa anashiriki mazungumzo naye kuhusu masuala mbalimbali ya kifamilia.

Alifichua kuwa huwa anajaribu kumweleza msichana huyo wa miaka tisa kuhusu hali nzima katika familia yake ili asishangae wakati akisoma mambo kwenye mitandao ya kijamii.

“Mtoto wangu ako na simu, ako na tablet. Shule pia wako na stori za internet. Kawaida mimi huwa na mazungumzo na mzaliwa wangu wa kwanza, amefikisha umri wa miaka tisa hivi majuzi. Kawaida huwa nashiriki mazungumzo naye kwa sababu kuna vitu atakutana nazo mitandaoni,” alisema.