Samidoh na Muigai wa Njoroge wavuana nguo jukwaani kuhusu kuachwa na wake zao (+video)

Haya yanajiri wakati waimbaji wote wawili hao wanadaiwa kuachwa na wake zao wa kwanza.

Muhtasari

•Walikuwa wakitumbuiza Embu wakati walipoamua kuchomeana kuhusu hali ya kutatanisha katika ndoa zao.

•Samidoh kwa ujasiri alijigamba kuwa tayari ameshapata pesa nyingi kiasi kwamba kwenda nje ya nchi ni kama kutembelea kijiji.

Samidoh na Muigai wa Njoroge
Image: INSTAGRAM// SAMIDOH

Waimbaji maarufu wa nyimbo za Kikuyu Samidoh Muchoki na Muigai wa Njoroge hivi majuzi walihusika katika mabishano ya kejeli wakati wa tamasha la moja kwa moja katika kaunti ya Embu.

Wawili hao walikuwa wakitumbuiza katika hoteli moja katika mji wa Embu wakati walipoamua kupeleka burudani yao katika kiwango kingine na kuwaburudisha mashabiki wao kwa kuchomeana kuhusu hali ya kutatanisha katika ndoa zao. Wasanii hao wawili wanadaiwa kuachana na wake zao wa kwanza.

Majibizano hayo ya kejeli yalianza baada ya Muigai wa Njoroge kusema kuwa anataka kwenda nyumbani kwa wake zake wawili ambao alidai walikuwa wakimsubiri.

“Si mmoja alitoroka!! *2” Samidoh alimjibu Muigai wa Njoroge.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili na za kisiasa hata hivyo alikanusha haraka madai hayo akisema kuwa hajawahi kupoteza mke, na kusisitiza kuwa wake zake huhama tu

“Si uliachwa *2, wakati tu ambapo umeongeza utamu..” Muigai alimwambia Samidoh.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za Mugithi alimjibu Muigai, “Walitoroka na ndege, walitoroka na ndege. Lakini wako alitoroka kwa pikipiki."

Muigai ambaye alionekana kutotikiswa na ‘tusi’ la mwenzake aliona ni faida akisema kuwa umbali mfupi kati yake na mkewe aliyetoroka ungemrahisishia kumrejesha akitaka.

“Wako ata ukimtaka *2, ni lazima utafute Visa,” Muigai alimwambia Samidoh na kuondoka jukwaani mara moja.

Samidoh kwa ujasiri alijigamba kuwa tayari ameshapata pesa nyingi kiasi kwamba kwenda nje ya nchi ni kama kutembelea kijiji.

Haya yanajiri wakati waimbaji wote wawili hao wanadaiwa kutengana na wake zao wa kwanza.

Kwa muda mrefu, Muigai wa Njoroge alikuwa kwenye ndoa iliyoonekana kuwa na furaha na wake wawili hadi mapema mwaka huu wakati habari zilipoibuka kuwa mke wa kwanza, Njeri alikuwa amegura ndoa  yao ya takriban mwongo mmoja na nusu.

Kwa upande mwingine, mke wa kwanza wa Samidoh Edday Nderitu alitangaza kugura ndoa yao ya zaidi ya miaka kumi mwaka jana alipohamia Marekani.