JuaCali afafanua maana halisi ya jina lake la kisanii

JuaCali amethibitisha kuwa jina lake halitokani na 'jua kali.'

Muhtasari

•JuaCali alishiriki mazungumzo ya kirafiki na watumiaji wa Twitter ambapo alifichua maelezo yasiyojulikana sana kuhusu jina lake la kisanii.

•Ilikuwa wakati huo ambapo alifichua kuwa jina lake ni ufupi wa msemo Jua California.

Image: INSTAGRAM// JUACALI

Siku ya Jumatatu, mwimbaji mkongwe wa Kenya Paul Julius Nunda almaarufu JuaCali alishiriki mazungumzo ya kirafiki na watumiaji wa mtandao wa Twitter ambapo alifichua maelezo yasiyojulikana sana kuhusu jina lake la kisanii.

Baba huyo wa muziki wa genge alikuwa amechapisha picha yake akiwa ndani ya gari na akatumia fursa hiyo kuwahimiza watu wengine pia kutoka nje.

“Siku nzuri nje, toka nje enjoy...,” JuaCali aliandika chini ya picha yake.

Shabiki mmoja alibaini jinsi nje inavyoonekana kung'aa na akaamua kumuuliza mwimbaji swali la kejeli.

“Ile Jua iko huko nje ndio kali ama ni wewe umewaka?” shabiki alijitambulisha kama Remmy aliuliza.

Rapa huyo akajibu, “Mimi ndio nimewaka.”

Mtumiaji mwingine wa Twitter alitaka kujua jinsi mwanamuziki huyo alivyobuni jina lake la kisanii la ‘JuaCali.’

Ilikuwa wakati huo ambapo alifichua kuwa jina lake ni ufupi wa msemo Jua California.

"JuaCali ina ufupi wa Jua California," alisema.

California ni mtaa katika jiji la Nairobi ambapo mwimbaji huyo wa genge anatoka.

JuaCali hajawahi kuona aibu kujihusisha na mizizi yake na mara nyingi ameonyesha hadharani jinsi anavyojivunia mahali alipotoka.

Mwaka wa 2000, pamoja na mtayarishaji wa muziki Clemo, walianzisha Calif Records ambapo amekuwa akitengeneza muziki ambao ulitawala kote Afrika Mashariki.

Lebo hiyo ya muziki pia ilipewa jina la California.