Hamisa Mobetto hatimaye afichua sababu ya kutengana na Mtogo Kevin Sowax

“Sina mahusiano. Mimi niko single sana. Ndiyo, siko katika mahusiano. Niko single,” Hamisa alisema.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alithibitisha kuwa muda umepita tangu alipoachana na mfanyibiashara huyo tajiri .

•Hamisa hata hivyo alimsifu mfanyibiashara huyo wa Togo huku akibainisha kuwa ataendelea kumthamini.

Kevin Sowax na Mpenzi wake Hamisa Mobetto
Image: INSTAGRAM// KEVIN SOWAX

Mwanamuziki na mwanamitindo mashuhuri kutoka Tanzania, Hamisa Mobetto amethibitisha kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Mtogo, Kevin Sowax.

Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa habari wa Tanzania, mama huyo wa watoto wawili alithibitisha kuwa muda umepita tangu alipoachana na mfanyibiashara huyo tajiri .

Alitaja umbali mrefu na shughuli zao nyingi kama baadhi ya sababu zilizowafanya kuchukua njia tofauti.

“Sina mahusiano. Mimi niko single sana. Ndiyo, siko katika mahusiano. Niko single,” Hamisa alisema.

Aliongeza, "Yule (Kevin) tuliachana. Tuliachana muda kidogo umepita, ilitrend kwenye mitandao ya kijamii. Hakukuwa kuna sababu haswa ya sisi kuachana tuseme sisi kama wenyewe lakini suala moja lilikuwa ni umbali, sote tuko mbali, yuko bize na mimi niko bize."

Licha ya kuachana, mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz hata hivyo alimsifu mfanyibiashara huyo wa Togo akibainisha kuwa ataendelea kumthamini.

"Ni mtu mzuri sana na ninamkubali, nitafanya hivyo kila wakati. Lakini ndivyo tu, njia zetu ilibidi zitengane kwa njia moja au nyingine. Ndio hivyo,” alisema.

Mwezi uliopita, Kevin Sowax ambaye anaendesha kampuni kubwa ya usafirishaji nchini China alionekana kuthibitisha kuvunjika kwa mahusiano yake na Hamisa wakati alipochapisha picha ya mwanamke mwingine anayeaminika kuwa mpenzi wake mpya.

Mfanyibiashara huyo alichapisha picha ya mwanamke mwenye mwili mzuri na kumtambulisha kama "Khadija Sowax."

Hata hivyo, alificha uso wa mwanamke huyo kwa maandishi.

Mapema mwaka huu, wawili walizua tetesi za kuachana baada ya Kevin kufuta picha zote za Mobetto kwenye mitandao yake ya kijamii.

Hamisa alimtambulisha Sowax kwa walimwengu alipomzawadia gari aina ya Range Rover. Wakati huo pia alimshukuru kwa kumnunulia gari hilo la kifahari.

“Yani kuna wanaume…alafu kuna mwanaume wangu mimi hapa. Asante, mpenzi…Nataka kulia. Asante kwa kunionyesha upendo wa kweli ni nini. Umekuwa kitu bora zaidi ambacho kimewahi kunitokea."

"Nakupenda weeh, roho yangu weee. Kwako sijiwezi…ohh mai Laaaavuuuu," aliongeza.

Baadaye, Sowax alifunguka kuhusu uhusiano wake na Hamisa.

“Tangu nilipokuona, nilijua kuwa wewe ndiye. Kadiri ninavyozidi kukufahamu ndivyo hisia zangu zinavyozidi kukua. Ninashukuru kuwa na wewe katika maisha yangu na kufurahia uzoefu wa siku zijazo," alisema.

Mobetto alisema anahisi kama amempata mpenzi wa maisha.

“Kwa muda nilikuwa najiona sina imani na ndoa, kipindi hicho sikuwahi kuona mfano wowote kuwa niwe na ndoa yangu kama mtu fulani na mke wake.

Lakini sasa naona umuhimu wa ndoa ukizingatia sasa nina watoto na najua umuhimu wa mume utakuwa hivi na hivi, sasa naona mifano naona vitu mitandaoni hadi najisikia kuolewa,” alisema mwanamitindo huyo.