Akothee akumbuka alivyozaa mtoto wa kwanza miezi 4 mapema akiwa na umri wa miaka 14

Mwanamuziki Akothee amefichua kuwa alijifungua mtoto wa kwanza ujauzito wake ukiwa na miezi 4 pekee.

Muhtasari

•Huku akitoa taarifa ya ziara yake katika hospitali ya Migori, Akothee alitumia fursa hiyo kueleza kuhusu uzoefu wake wa uzazi.

•"Nilipata mzaliwa wangu wa kwanza katika wiki 20 na nilikaa hospitalini kwa miezi minne," Akothee alifichua.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Jumanne, mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Migori ambako aliangalia hali ya kituo hicho cha afya, akatangamana na wagonjwa na wanawake wanaojifungua katika wadi ya uzazi.

Mjasiliamali huyo mwenye umri wa miaka 43 alisifu hali ya hospitali hiyo, hasa sehemu ya uzazi ambayo alisema ni kisafi na kinatunzwa vizuri.

Huku akitoa taarifa ya ziara yake katika hospitali hiyo siku ya Jumanne, mama huyo wa watoto watano alitumia fursa hiyo kueleza kuhusu uzoefu wake wa uzazi.

"Nilipata mzaliwa wangu wa kwanza katika wiki 20 na nilikaa hospitalini kwa miezi minne. Nilikuwa na umri wa miaka 14 pekee kwa hivyo unajua ninahusiana vyema na uzazi,” Akothee alisimulia.

Mwimbaji huyo alionekana kuvutiwa sana na hali ya hospitali hiyo ya Kaunti ya Migori na hata akadokeza kwamba anaweza kuchagua kujifungulia katika wadi yake ya uzazi akipata ujauzito.

“Wow, sasa naweza kupata ujauzito. Nilipata fursa ya kuzuru Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Migori leo,” alisema.

Aliongeza, "Nilitembelea Kituo hicho kizima cha afya. Na niamini sikuwahi kufikiria kuwa ipo. Kitengo cha uzazi ni safi kwani unaweza kuona kikiwa na nafasi nzuri, na sehemu ya kushangaza zaidi ilikuwa kitengo maalum, ambapo watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wanashughulikiwa. Nilichokiona leo kilinipa matumaini kwa akina mama.”

Haya yanajiri kipindi ambapo mama huyo wa watoto watano amekuwa akidokeza  kuhusu kupata mtoto na mumewe Denis Shweizer almaarufu Omosh.

Takriban miezi miwili iilyopita, mwanamuziki huyo alidokeza  kwamba ameanza maandalizi ya safari yake ya ujauzito.

Mama huyo wa watoto watano kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyesha pakiti ya dawa aina ya Pregnacare Plus Omega-3 ambayo kwa kawaida hutumiwa na wanawake wakati wa safari ya ujauzito.

"Yoooo safari inaanza sasa NDILAS," Akothee alisema chini ya video fupi ya dawa hizo ambayo alichapisha.

Hii ilikuwa siku chache baada ya mwimbaji huyo kutangaza mpango wa kuchukua mapumziko kutoka kwa mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake ya mwezi Aprili, mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa madhumuni ya mapumziko yake ya muda usiobainishwa yangekuwa kuangazia kuongeza mtoto mwingine na mume wake Omosh.

Aliwaomba mashabiki wake wamruhusu achukue mapumziko akisema anataka kupata mtoto wake wa sita hivi karibuni.

"Sasa nyie mnipe muda. Nitapumzika kutoka kwa kila mtu na kila kitu pamoja na mitandao ya kijamii. Mniruhusu nitafute mtoto wangu wa pili kutoka mwisho, kabla hatujazungumza mambo mengine.  Nataka kuwa mama mwaka huu," Akothee alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.