Akothee aweka mambo bayana kuhusu iwapo ana mipango ya kisiasa

Akothee aliwabainishia wanasiasa wa Migori kwamba hapangi kuchukua viti vyao kwani hana nia ya siasa.

Muhtasari

•Akothee aliweka wazi kuwa licha ya kuhusika kwake na masuala ya kaunti ya Migori, hana nia ya kuchukua wadhifa wowote.

•Alisema yeye si shindano la mwanasiasa yeyote na kuweka wazi kuwa yeye ni balozi wa kaunti anayefanya kazi yake.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali maarufu wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee ameweka wazi kuwa hana nia yoyote ya kujihusisha na siasa za kaunti.

Katika taarifa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa licha ya kuhusika kwake na masuala ya kaunti ya Migori, hana nia ya kuchukua wadhifa wowote.

Alibainisha kuwa amekuwa akitumia tu chapa yake kutekeleza majukumu yake kama balozi wa wa Kaunti ya Migori wala sio kujihusisha na siasa.

"Siko Migori kuchukua nafasi ya mtu yeyote., Sina nia ya siasa za kaunti, nafanya kazi ninayofanya vizuri na niliyoteuliwa 🙏. mapenzi inikoseshe usingizi na halafu local side shows za politics pia iniitoe roho!!,” Akothee alifoka kwenye Instagram.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye amezingirwa na drama nyingi alikuwa akiwahutubia wanasiasa wa kaunti ya Migori na kuwasuta kwa kuzembea sana kwenye kazi zao.

Pia aliwabainishia wanasiasa wa kaunti hiyo yake ya nyumbani kwamba hapangi kuchukua viti vyao kwani hana nia ya siasa.

“Kwa Mara nyingine tena sina nia yoyote katika siasa, siijui wala muundo wake. Mnikomeeee,” alisema.

Aliweka wazi kuwa hatakubali kutishwa wala kuzuiwa na mtu yeyote huku akibainisha kuwa alijenga chapa yake nje ya siasa.

Aliendelea kubainisha kuwa yeye si shindano la mwanasiasa yeyote na kuweka wazi kuwa yeye ni balozi wa kaunti anayefanya kazi yake.

“Nimezaliwa na kukulia katika kaunti ya Migori, niliolewa Kamagambo, watoto wangu wanapiga kura katika kaunti ya migori. Nina haki zangu za kidemokrasia. Na chapa ya kulinda. Tuheshimiane,” aliwaambia wanasiasa hao.

Mwimbaji huyo alielezea kusikitishwa kwake na wanasiasa wa kaunti yake ya nyumban akibainisha kuwa baadhi yao tayari wameanza kufanya kampeni za 2027.

“Siasa mbaya za Migori zimeathiri watu wetu, hakuna wa kuwaonyesha njia sahihi ya siasa, tumepoteza vitega uchumi, wawekezaji kutokana na siasa zetu mbovu. Tuwe wangwana .Tunataka viongozi wanaojiamini sio wale wanaohisi kutishwa na watu wanaojali mambo yao binafsi," alisema.