Akothee hatimaye afunguka kuhusu kuvunjika kwa ndoa na Omosh, kwa nini alitoroka

Akothee alifichua aligura ndoa yake wakati wa fungate baada ya kujua mambo ambayo hakujua hapo awali.

Muhtasari

•Akothee alithibitisha kwamba aligura ndoa yake ya muda mfupi mnamo mwezi Juni wakati yeye na Omosh walipokuwa kwenye fungate.

•Akothee alidokeza kwamba hakumwambia mumewe kuhusu uamuzi wake mara moja na hata alimdanganya kwamba hangemuacha.

wakifurahia fungate jijini Santorini, Ugiriki.
Akothee na aliyekuwa mumewe Denis Shweizer wakifurahia fungate jijini Santorini, Ugiriki.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Msanii na mfanyibiashara mashuhuri wa Kenya, Esther Akoth almaarufu Akothee amethibitisha kuwa ndoa yake na Denis ‘Omosh’ Schweizer tayari imevunjika.

Akothee alithibitisha uvumi ambao umekuwa ukienea kwa muda mrefu sasa Jumanne usiku aliposhiriki kipindi cha moja kwa moja na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Katika kipindi hicho, mama huyo wa watoto watano alithibitisha kwamba aligura ndoa yake ya muda mfupi mnamo mwezi Juni wakati yeye na Omosh walipokuwa kwenye fungate.

“Nimehama kutoka kwa mahusiano hayo. Hayapo tena. Ninataka kuwaaambia kwamba nilitoka kwenye uhusiano huo mwezi Juni. Hata hivyo sitaeleza kwa undani,” Akothee alisema.

Aliongeza, “Nilifurahia ndoa yangu, nilifurahia harusi yangu. Sijutii chochote. Nilifanya harusi yangu mnamo siku ya kuzaliwa kwangu ndio ikiwa tu mambo yangeenda vibaya, kama wamefanya, basi singekuwa na majuto yoyote.”

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alidokeza kwamba aligura ndoa yake walipokuwa wakifurahia fungate yao baada ya kujifunza mambo kadhaa ambayo hakujua hapo awali.

Hata hivyo alidokeza kwamba hakumwambia mzungu huyo kutoka Uswizi kuhusu uamuzi wake mara moja na hata walipokuwa wakiagana, alimdanganya kwamba hangemuacha.

"Nilitoka nje ya uhusiano mnamo Juni. Kawaida mimi hutoka nje ya uhusiano wangu wakati bado niko kwenye uhusiano. Tulipokuwa kwenye fungate, niligundua mambo fulani ambayo sikuweza kustahimili. Kisha akaniuliza, “Utaniacha?” Nikasema, "hapana mpenzi nakupenda". Nilipokuwa nikitoka Uswizi mnamo Julai, kwenye uwanja wa ndege aliniuliza," utaniacha?, Nikasema "hapana mpenzi, nakupenda". Lakini kwa hakika, nilikuwa tayari nimeondoka,” Akothee alisimulia.

Muimbaji huyo ambaye maisha yake yamejawa na drama aliweka wazi kuwa kwa sasa yuko single akibainisha kuwa hakuna wakati hata ataruhusu mwanaume kumuathiri kisaikolojia.

“Mimi ni mtu ambaye silazimishi mambo. Wakati haifanyi kazi kwangu, hata ikiwa inakufanyia kazi, haifanyi kazi. Sababu ya kutodumu katika mahusiano yenye sumu ambayo sielewi ni kwa sababu pesa zangu ziko kichwani mwangu. Wakati ninapomruhusu mwanaume yeyote kunichafua kichwa, basi ananivuruga mfukoni,” alisema.

Aliongeza, "Sitaomba msamaha kwa chochote, ikiwa uhusiano haukufanya kazi kwangu, ningefanya nini?. Haikufanya kazi, ilifanya kazi siku chache, wakati mask ilianguka, sikuweza kubaki pale. Nilikuwa nikibaki pale kwa ajili ya nini? Kufikia wakati humkuwahi kumuona Denis kwenye akaunti zangu za mitandao ya kijamii, ni wakati ambao nilikuwa nasimamia wakati wa kuondoka kwangu."