Diana Marua awajibu wanaomuonya kuwa mumewe atampachika Yvette ujauzito wa pili

Diana alibainisha kuwa ataendelea kumkubali Yvette kuwa sehemu ya familia yake

Muhtasari

•Diana hata hivyo ameweka wazi kuwa hana nia yoyote ya kukatiza uhusiano wake mzuri na Mama Mueni.

•Alifichua kuwa baby mama huyo wa mumewe tayari yupo kwenye mahusiano mengine ambayo yeye na Bahati wanaheshimu.

Yvette Obura na Diana Marua
Yvette Obura na Diana Marua
Image: YOUTUBE// DIANA MARUA

Msanii Diana Marua almaarufu Diana B ameendelea kuwakosoa wanamitandao wanaopinga ukaribu wake na aliyekuwa mpenzi wa mumewe, Yvette Obura.

Baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakimshauri dhidi ya  urafiki na Yvette huku baadhi wakimuonya kuwa huenda hisia za mumewe kwa mzazi huyo mwenzake zikafufuka na hata wakapata mtoto mwingine pamoja.

Diana hata hivyo ameweka wazi kuwa hana nia yoyote ya kukatiza uhusiano wake mzuri na Mama Mueni.

"Nashangaa wanataka nifanye nini. Nichukue bwana yangu nimfungie mahali? Mwisho wa siku tunaishi katika mazingira ya kuheshimiana kwa pande zote mbili. Anaheshimu nafasi yangu, naheshimu nafasi yake na Bahati anatuheshimu sote wawili," Diana alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alibainisha kuwa ataendelea kumkubali Yvette kuwa sehemu ya familia yake kwa kuwa ni mama wa binti ya mumewe, Mueni Bahati, ambaye anaishi naye kwa sasa.

Diana alifichua kuwa baby mama huyo wa mumewe tayari yupo kwenye mahusiano mengine ambayo yeye na Bahati wanafahamu kuhusu na kuyaheshimu.

"Yupo karibu kwangu. Anaheshimu mahusiano yangu na Bahati. Yeye pia ako na mahusiano yake mahali alipo,  na tunaheshimu hilo. Wakati mwingine ata akimleta Mueni  huwa anakuja na mpenzi wake na tunaheshimu hilo. Mengine ambayo watu wanasema ni kelele tu ya nyuma," Alisema.

Alieleza kuwa uhusiano wao mzuri ulianza baada ya Mama Mueni kubaini kuwa nafsi yake ni safi na hana nia yoyote mbaya.

Mwezi uliopita Diana aliwaomba wanamitandao kutoingilia maisha yake ya kibinafsi  baada ya shabiki mmoja kumuonya kuwa huenda mumewe na Yvette wakapata mtoto wa pili pamoja ikiwa ataendeleza urafiki naye.

'Diana, narudia tena.. utajuta, ni muda tu, mtoto wake wa pili atakuwa wa Bahati kwa mara nyingine,"  Mtumiaji mmoja wa Instagram wa kike alimuonya Diana.

Mkewe Bahati alimtaka shabiki  huyo kutoingilia mambo ya kwake huku akidokeza angekubali kama hilo lingetokea.

"Kila mtu afagie kwake. Watoto ni baraka ama?" Diana alimjibu.

Hii ilitokea baada yake kupakia video ikimuonyesha Yvette akiwa amemshika bintiye ,Heaven Bahati, ambaye alifurahiwa kuwa karibu naye.

Katika chapisho hilo, Diana alifanya mzaha kuhusu hilo huku akidai kuwa binti yake alikuwa amepata mama mpya.