"Kila mtu afagie kwake!" Diana akataa ushauri wa kukatiza urafiki na aliyekuwa mpenzi wa Bahati

Muhtasari

•Mkewe Bahati alimtaka mwanadada huyo kutoingilia mambo ya kwake huku akidokeza angekubali kama hilo lingetokea.

Yvette Obura na Diana Marua
Yvette Obura na Diana Marua
Image: YOUTUBE// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua ameweka wazi kuwa hana nia ya kukatiza urafiki wake na mpenzi  wa zamani wa Bahati, Yvette Obura.

Jumatatu, mama huyo wa watoto wawili alipakia video ikimuonyesha Yvette akiwa amemshika bintiye Heaven Bahati.

Heaven alionekana kufurahia kuwa karibu na baby mama huyo wa babake na hata alisikika kwenye video akisema kuwa yeye ni mama yake.

"Mueni ni dadake na mimi ni mtoto wake. Nitaenda naye," Heaven alimwambia mamake baada ya kumuomba amruhusu Mama Mueni aende kwao.

Katika chapisho lake, Diana alifanya mzaha kuhusu hilo huku akidai kuwa binti yake alikuwa amepata mama mpya.

"Hivyo tu.. Heaven Bahati amepata mama mwingine. Anasema Mama Mueni ni mama yake na mimi ni nani niseme neno?," Diana aliandika chini ya video aliyopakia.

Kama ilivyo ada, mamia ya mashabiki wake walifurika chini ya chapisho hilo na kutoa hisia mseto.

Huku mashabiki wengi wakionekana kupongeza uhusiano mzuri kati ya wazazi hao wa watoto wa  Bahati, mmoja wao hata hivyo alivutia umakini wa Diana baada ya kumshauri dhidi ya urafiki huo.

"Diana, narudia tena.. utajuta, ni muda tu, mtoto wake wa pili atakuwa wa Bahati kwa mara nyingine,"  Mtumiaji mmoja wa Instagram wa kike alimuonya Diana.

Mkewe Bahati alimtaka mwanadada huyo kutoingilia mambo ya kwake huku akidokeza angekubali kama hilo lingetokea.

"Kila mtu afagie kwake. Watoto ni baraka ama?" Diana alimjibu mwanadada huyo.

Takriban miezi miwili iliyopita Diana na Obura walishirikimazungumzo ya pamoja ambapo walifichua kuwa walizozana kwa muda kabla ya kuwa marafiki.

Katika mazungumzo hayo Diana alifichua kuwa ugomvi wake na Yvette ulianza baada yake kupakia picha aliyopigwa pamoja na binti ya Yvette.

"Mimi nilipost picha tu. Wanamitandao walianza kunishambulia wakisema ningemuuliza mamake kwanza. Kulikuwa na mambo mengi. Nilisema uharibifu umeganyika tayari na hakuna kitu ambacho ningeweza kufanya. Nilidhani kitu cha maana kufanya ni kufanya ni kufuta picha lakini Baha alisema nisifute. Hapo ndipo beef ilianza rasmi. Nadhani mimi ndio nilichokoza nyuki," Diana alisema.

Baada ya wawili hao kutofautiana kuhusu kulizuka mvutano kati yao kwa muda kabla ya  kukubaliana kusuluhisha mizozo yao.

Yvette alifichua alimfikia Diana kupitia mtandao wa Instagram akiomba msamaha kwa yaliyotokea kati yao.

"Nilichukua simu yangu nikakuandikia (Bahati), 'Umekuwa mama mzuri kwa  Mueni kutokana na yale  ambayo huwa ananiambia. Pole kama nimewahi kukosea ama kufanya maisha yako yawe mazuri. Nisamehe na ningetaka tuwe mahali pazuri'. Kusema kweli sikudhani ungejibu," Yvette alimwambia Diana.

Wawili hao walifichua kuwa walilazimika kushirikiana katika malezi ya Mueni baada ya Bahati kuwaagiza wawe wanawasiliana.