Diana Marua azungumzia kuhusishwa na Omanyala & Wanyama, kwa nini Morgan ni baraka

Alisema halaumu watu kwa kumhusisha na wanaspoti hao akibainisha kuwa kila mtu ana maoni yake.

Muhtasari

•Diana aliweka wazi kuwa hata hamfahamu Omanyala na kubainisha kuwa amemuona tu akikimbia kwenye runinga.

•Diana alisema alikutana na Bahati baada ya maisha yake ya zamani ya uchumba na wakaanza kuchumbiana na kupendana.

Image: Diana Marua// INSTAGRAM

Mwanavlogu maarufu wa Kenya Diana Marua hivi majuzi alishiriki mazungumzo ya wazi na wasaidizi wake wa nyumbani ambapo alijibu kuhusu baadhi ya masuala yanayowapa wasiwasi kuhusu maisha yake ya kibinafsi, familia na taaluma yake.

Miongoni mwa masuala ambayo alilazimika kuzungumzia ni mashambulizi ya mtandaoni ambapo mwanawe wa kulea Morgan Bahati alihusishwa na wanamichezo maarufu wa Kenya Ferdinand Omanyala na Victor Wanyama.

Katika majibu yake, mama huyo wa watoto watatu aliweka wazi kuwa hata hamfahamu Omanyala na kubainisha kuwa amemuona tu akikimbia kwenye runinga.

“Mimi sijawahi kupatana na Omanyala. Huwa namuona tu akikimbia kwa TV. Huwa namuona akishinda tuzo za Olimpiki. Hivyo ndo namjua Omanyala. Hivyo ndivyo sivyo kabisa,” Diana Marua alisema.

Alisema kuwa hawalaumu Wakenya kwa kumhusisha na wanaspoti hao akibainisha kuwa kila mtu ana maoni yake kuhusu kila kitu.

Alisema alikutana na mwimbaji Kelvin Bahati baada ya maisha yake ya zamani ya uchumba na wakaanza kuchumbiana na kupendana.

“Vile nilipatana na Baha nilipata kama ameadopt watoto. Kati ya watoto hao watatu kulikuwa na Morgan, Purity na Rose. Wote walikuwa kwa Children’s Home,” alisema.

Alisimulia jinsi mume wake alivyomchukua Morgan kutoka kwa Nyumba ya Watoto ambako pia yeye alikulia baada ya kuvutiwa naye. Mvulana huyo alikuwa na umri wa miaka miwili pekee wakati mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alipomchukua kuwa mwanawe.

“Nilipokutana na Bahati na hao watoto, nilimpenda hivyo. Ukipenda mtu,unapenda mtu na watu wao. Nilikuwa tayari kutulia na Bahati na watu wake,” alisema.

Aliongeza, “Mimi kusema hivyo, ninajivunia sana na ninaheshimika kuwa mama ya Morgan. Hakika yeye ndiye mtu wa kwanza kuwahi kuniita mama. Yeye ndiye alinipa jina mama. Na kila wakati mimi ninajivunia hilo.

Rapa huyo alifichua kuwa anaamini mafanikio yote ambayo yeye na Bahati wamepata katika miaka kadhaa ya ndoa yao ni baraka zilizoletwa na Morgan.

"Bila shaka imekuwa si rahisi kumlea Morgan lakini mahali tumefika saa hii ni Mungu," alisema.

Bahati alimchukua Morgan kuwa mwanawe mwaka wa 2013 wakati alipotembelea chumba cha watoto cha ABC ambapo alikulia pia.