Edday Nderitu akataa kubanduka, ashikilia msimamo wake kuhusu Karen Nyamu kuwa mke mwenzake

Mama huyo wa watoto watatu hana uhusiano mzuri na mpenzi wa mumewe, Karen Nyamu.

Muhtasari

•Edday Nderitu ameweka wazi kuwa habanduki kutoka msimamo wake wa awali wa kutokubali kuwa na mke mwenza.

•Karen Nyamu alisema atakuwa sawa kuwa na mke mwenza ikiwa Edday Nderitu na mwimbaji Samidoh watafufua ndoa yao.

Edday Nderitu.
Edday Nderitu.
Image: FACEBOOK// EDDAY NDERITU

Mke wa kwanza wa mwimbaji wa Mugithi Samidoh, Bi Edday Nderitu amesisitiza msimamo wake kuhusu kuwa katika ndoa ya wake wengi.

Mama huyo wa watoto watatu ambaye amekuwa akiishi Marekani kwa miezi kadhaa iliyopita alikuwa akimjibu mwanamtandao mmoja mnamo siku ya Jumatatu alipoweka wazi kuwa habanduki kutoka msimamo wake wa awali wa kutokubali kuwa na mke mwenza.

Mtumiaji wa Facebook alikuwa ametoa maoni katika chapisho lake akimtaka kukubali tu kushirikiana katika malezi na Samidoh lakini asigawane na mwanamke mwingine.

"Natumai utashikamana na maneno ya mshauri wako "Hakuna ku’share, lakini kuna uzazi mwenza," Purity Amani alitoa maoni chini ya moja ya machapisho ya Edday.

Edday  alijibu, "Ninashikilia neno langu, ku’share kamwe hakutatokea."

 Haya yanajiri siku chache tu baada ya mpenziwe Samidoh, seneta Karen Nyamu kudokeza kuwa atakuwa sawa kuwa na mke mwenza ikiwa Edday Nderitu na mwimbaji huyo watafufua ndoa yao.

Mwanasiasa huyo alitoa maoni hayo alipokuwa akifichua kuwa staa huyo wa Mugithi yuko nchini Marekani kutembelea familia yake ambayo imekuwa ikiishi huko.

 “Yeye (Samidoh) yupo huko tunapozungumza kuona watoto. Edday pia akirudi kwa mix timeshare miaka mingi sana kwa amani, kamwe hatawahi kuwa tatizo,” Karen Nyamu alisema alipokuwa akimjibu shabiki katika chapisho la hivi majuzi la Facebook.

Image: FACEBOOK// EDDAY NDERITU

Mke wa Samidoh wa miaka mingi, Edday Nderitu kwa sasa anaishi Marekani pamoja na watoto wao. Aliondoka nchini mapema mwaka jana na anaonekana tayari kutulia huko vizuri huku watoto wakiwa wameanza shule huko.

Mwezi Julai mwaka jana, Bi Edday Nderitu aliweka wazi kwamba alimuacha mumewe ili awe na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."