Esther Musila akagua jumbe za MPESA za Guardian Angel baada ya kuambiwa anam'cheat, "atakuletea ugonjwa"

Bi Musila aliambiwa mumewe alikuwa akimcheza na binti ya mwanasiasa na walikuwa wakikutana katika chumba cha wageni.

Muhtasari

•Bi Musila alisimulia jinsi mwanamke tapeli alivyojaribu kumlaghai pesa kwa kudanganya kuhusu Guardian Angel kucheza karata nje ya ndoa.

•Baada ya Bi Musila kusema atafanya uchunguzi wake, mwanadada huyo alimtaka amlipe ‘tokeni’ kwa habari alizompa.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mke wa mwimbaji Guardian Angel, Bi Esther Musila amesimulia kuhusu tukio la kutia wasiwasi na la kushtua ambalo alikumbana nalo siku ya Jumatano.

Katika video iliyoshirikiwa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, mama huyo wa watoto watatu alisimulia jinsi mwanamke tapeli alivyojaribu kumlaghai pesa kwa kudanganya kuhusu Guardian Angel kucheza karata nje ya ndoa.

Musila alisimulia jinsi mwanamke aliyedai kuwa mbunge katika bunge la EALA na mmiliki wa nyumba ya wageni maalum alivyomtafuta akidai kuwa na ushahidi wa mumewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanadada mwingine. Alisoma ujumbe ambao mwanamke huyo alimtumia.

Ujumbe huo ulisomeka, “Unaonekana kuwa mwanamke mwenye heshima, mnyenyekevu, mwenye akili timamu, anayemcha Mungu na mwenye upendo. Je, hivi majuzi umemshuku mwanamume wako na mwanamke mwingine? Nadhani hustahili hii. Yaani ameona tu akucheze na aina hiyo!! Au amemchagua juu ako na makalio makubwa? Huyu atakuletea ugonjwa bure! Ninamiliki nyumba ya watu mashuhuri na kwa hivyo ninaweza kufikia picha za CCTV na malipo ya MPESA. Natumai hii itakuwa kati yangu na wewe. Hutafichua chanzo cha habari,”

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alisema kuwa mwanamke ambaye aliwasiliana naye alisisitiza kwamba alikuwa na ushahidi wa kutosha kuwa mume wake alikuwa akim’cheat na hata akaendelea kushiriki ujumbe wa miamala ya MPESA ya Guardian Angel akidaiwa kulipia chumba cha wageni cha VIP. Tapeli huyo alidai kuwa mwanamke ambaye mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alikuwa na uhusiano wa kimapenzi naye ni binti wa mwanasiasa.

"Wakati wa mazungumzo, alikuwa akiniambia "unajua, hii sio haki kwako". Nilimwambia, “Nina umri wa miaka 53, sitawahi kufuatilia mwanamume. Chochote anachotaka kufanya, anaweza kukifanya. Hakuna ninachoweza kuzuia”. Alisema hataki nimfichue. Nilimwambia kuwa nitafanya uchunguzi wangu mwenyewe hana haja ya kuwa na wasiwasi,” alisema.

Ni baada ya Bi Musila kusema kuwa atafanya uchunguzi wake mwenyewe ambapo mwanadada huyo alimtaka amlipe ‘tokeni’ kwa habari alizompa.

Baada ya kufanya uchunguzi wake na hata kuangalia simu ya Guardian Angel ili kuthibitisha kama jumbe za miamala ya MPESA alizotumiwa zilikuwa za kweli, mama huyo wa watoto watatu hata hivyo aligundua kuwa madai hayo yote yalikuwa ya uwongo.