Eve Mungai avunja kimya baada ya Director Trevor kumtimua kutoka Mungai Eve Media

Jumatatu, Director Trevor alitangaza kwamba huduma za Eve Mungai hazitahitajika tena katika Mungai Eve Media.

Muhtasari

•Eve Mungai alionekana kutosumbuliwa hata baada ya Director Trevor kutangazaa kwamba walikuwa wametengana kikazi.

•Eve alionekana kufurahia idadi kubwa ya watazamaji waliokuwa wakifika kwenye ukurasa wake, pengine wakitarajia kuona majibu yake.

Director Trevor na Mungai Eve
Image: HISANI

Mtayarishaji maudhui Eve Mungai alionekana kutosumbuliwa hata baada ya mpenzi wake wa muda mrefu Bonaventure Monyancha almaarufu Director Trevor kutangaza kwamba walikuwa wametengana kikazi.

Siku ya Jumatatu, Trevor kupitia ukurasa wake wa Instagram alifichua kuwa alikuwa akibadilisha Mungai Eve Media kuwa Kenya Online Media. Alitangaza zaidi kuwa huduma za Mungai Eve hazitahitajika tena kwenye chaneli za YouTube na akaunti za mitandao ya kijamii anazosimamia.

Wanamitandao wa Kenya wenye shauku walisubiri kwa hamu kuona jinsi mrembo huyo wa miaka 23 angepokea habari ambazo mpenzi wake wa muda mrefu alikuwa ametangaza. Hata hivyo alionekana kutotikiswa na alishiriki tu kuhusu safari ya peke yake ambayo alikuwa akisafiri kwenda Zanzibar.

"Siku zote nilitaka kufanya likizo za peke yangu na nina furaha sana @bonfireadventures inafanikisha," Mungai Eve aliandika chini ya video moja ikimuonyesha katika chumba chake cha hoteli.

Pia alishiriki picha nzuri ikimuonyesha akiwa uwanja wa ndege tayari kwa likizo iliyokuwa mbele yake.

Mtayarishaji wa maudhui huyo hata hivyo alionekana kufurahia na kujivunia idadi ya watazamaji waliokuwa wakifika kwenye ukurasa wake, pengine wakitarajia kuona majibu yake.

"Siku nzuri ya kuweka matangazo yako nami.. Eeeiy, nawaona wote," aliandika chini ya screenshot zinazoonyesha maelfu ya watumiaji wa mtandao ambao walikuwa wametembelea ukurasa wake wa Instagram.

Siku ya Jumatatu jioni, Director Trevor ambaye jina lake halisi ni Bonaventure Monyancha alitangaza mabadiliko kadhaa makubwa katika kampuni ya Mungai Eve Media ambayo yatatekelezwa Jumanne, Februari 20

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alitangaza kuwa kampuni hiyo ya habari za mitandaoni itabadilisha jina lake kuwa Kenya Online Media.

"Je, uko tayari? Taarifa rasmi itashuka kesho," Director Trevor alitangaza.

Alifichua kuwa kutakuwa na mabadiliko kwenye chaneli za YouTube za Mungai Eve na Insta Fame zenye jumla ya wafuasi zaidi ya 850,000 pamoja na ukurasa wa Facebook wa Mungai Eve Media wenye takriban wafuasi 874,000

Wakati alipoulizwa ikiwa ataendelea kufanya kazi na mpenzi huyo wake wa muda mrefu, Trevor alisema kuwa huduma zake hazitahitajika tena.

"Hapana! Huduma zake hazihitajiki tena kwenye mifumo ifuatayo, YouTube – wanaofuatilia 754k, wanaofuatilia Insta Fame 104k, Facebook 874k," alisema.

Katika taarifa nyingine, mtaalam huyo wa mitandao ya kijamii alionekana kumrushia vijembe Mungai Eve akidokeza kuwa mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23 anafurahia matunda ya mti alioupanda muda mrefu uliopita.

"Kuna mtu ameketi kivulini leo kwa sababu mtu alipanda mti muda mrefu uliopita," aliandika.

Hatua ya hivi punde ya Director Trevor ilizidisha tetesi za kuachana kwao ambazo zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni.