Fahamu kwa nini mahusiano Vera Sidika hayakuwahi kudumu zaidi ya miezi 6

Vera alidai kwamba hapo awali aliwahi kuwa kwenye mahusiano matatu pekee.

Muhtasari

•Vera anaaminika kuwahi kuchumbiana na wanaume kadhaa kabla ya hatimaye kutulia kwenye ndoa na mwimbaji Brown Mauzo.

•Vera aliweka wazi kuwa anafurahia ndoa yake na Mauzo ambayo sasa imedumu kwa takriban miaka miwili unusu.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti maarufu Vera Sidika ni miongoni mwa watu mashuhuri Wakenya ambao wamekuwa na maisha ya mapenzi yenye utata zaidi.

Vera anaaminika kuwahi kuchumbiana na wanaume kadhaa kabla ya hatimaye kutulia kwenye ndoa na mwimbaji Brown Mauzo. Miongoni mwa wanaume ambao amewahi kuhusishwa nao hapo awali ni pamoja mwanamuziki Otile Brown, mfanyibiashara Yommy Johnson kutoka Nigeria na daktari wa Tanzania Jimmy Chansa.

Mama huyo wa binti mmoja alishiriki mahojiano na Massawe Japanni alidai kwamba hapo awali aliwahi kuwa kwenye mahusiano matatu pekee.

"Kwa jumla naweza kusema niko na ex kama watatu," alisema.

Vera aliweka wazi kwamba amekuwa mwaminifu katika mahusiano yote ambayo amekuwa nayo. Hata hivyo, alibainisha kuwa wakati wa kuondoka ukifika, yeye hubeba hisia zake zote na huwa haangalii nyuma tena kamwe.

Alisema anapokuwa akichumbiana na mtu huwa anawekeza hisia zake zote kwenye mahusiano hayo na anapokosewa huwa hachukulii kirahisi.

"Huwa nakwamilia kwa mtu mmoja. Kamwe huwa sicheat. Ni jambo ambalo ex wangu wote wanaweza kuthibitisha," alisema.

Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 alikiri kuwa hakuna mahusiano yake ya awali yaliyodumu  zaidi ya miezi sita.

Alieleza kwamba kwa kawaida alikuwa akitumia miezi michache ya kwanza ya mahusiano yake kusoma tabia na mienendo ya mpenzi wake na kubaini kama kwamba wana kuna uwezekano wa wao kuwa wenzi wa maisha. 

"Miezi sita iliweza kunijulisha ikiwa mahusiano yanaenda mahali au la. Mimi sio mtu wa kupenda kupoteza wakati. Siwezi kutaka kupoteza wakati wangu mahali ambapo naona hakuna future. Siwezi kaa kwenye mahusiano kwa miaka mbili au tatu na najua vizuri hakuna mahali ambapo tunaenda," alisema.

"Ikifika miezi tatu mtu huwa ameanza kuona mtu ni wa aina gani. Miezi ya kwanza mtu anaweza kujifanya. Lakini miezi ya  tatu, nne tano unaanza kuona ukweli. Kwangu ikifika miezi mitano nilikuwa najua mtu ako vipi,"

Vera aliweka wazi kuwa anafurahia ndoa yake na Mauzo ambayo sasa imedumu kwa takriban miaka miwili unusu.

Alikiri kuwa aliwahi kuvunjwa moyo katika siku za nyuma.