Fahamu sababu kuu ya Harmonize kumjengea mama yake jumba zuri la kifahari

Harmonize alionyesha jumba kubwa zuri la kifahari ambalo anaendelea kumjengea mama yake mzazi.

Muhtasari

•Konde Boy aliapa kwamba hatakata maji kamwe tena hadi wakati atakapokamilisha kujenga jumba la kifahari la mama yake kipenzi.

•Konde Boy alibainisha kuwa wakati mwingine mtu hufeli katika maisha na anahitaji mahali pa kurudi.

ameonyesha jumba la kifahari analomjengea mama yake.
Harmonize ameonyesha jumba la kifahari analomjengea mama yake.
Image: HISANI

Siku ya Jumanne, staa wa bongo fleva Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize alionyesha jumba kubwa zuri la kifahari ambalo anaendelea kumjengea mama yake mzazi.

Katika sehemu ya maelezo ya video hiyo, mwimbaji huyo mahiri alidokeza kuwa hakutumia siku akinywa pombe bali alidokeza kuwa alitumia sehemu kubwa ya siku hiyo akikagua maendeleo ya jengo la ghorofa moja ambalo bado linaendelea kujengwa.

Konde Boy aliapa kwamba hatakata maji kamwe tena hadi wakati atakapokamilisha kujenga jumba la kifahari la mama yake kipenzi.

“Leo sijalewa nimefanya mambo ya msingi sanaa. Hongera Mama Konde sinywiii tena mpaka nimalizie kinyumba chako,” Harmonize alisema.

Wakati huo huo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliendelea zaidi kufichua sababu kuu ya kwa nini anaangazia kumjengea mama yake nyumba ambapo alidokeza kuwa hakuna mtu anayejua kitakachotokea kesho.

Konde Boy alibainisha kuwa wakati mwingine mtu hufeli katika maisha na anahitaji mahali pa kurudi, ambapo kwa upande wake itakuwa ni katika nyumba ya mama yake.

“Ya dunia ni mengi na walimwengu nao wanamuomba Mungu!! Nae hana hiyana muda mwingine anawapa mambo yaki, kaa vibaya nahamia kwako Mama Konde. Sijalewa na silewi tena,” alisema Harmonize.

Staa huyo wa bongo fleva hapo awali  ametangaza kwamba ameacha kabisa kubugia mvinyo huku akiahidi kutolewa tena.

Katika taarifa fupi siku  ya Jumanne, staa huyo wa bongo fleva alimwomba Mungu amsaidie anapoanza maisha bila pombe.

“Natangaza rasmii nimeacha pombe. Sinywii tenaa. Maisha Mungu Nisimamie,” Harmonize alisema kwenye Instagram.

Tangazo hilo lilikuja siku chache tu baada ya mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ kubugia mvinyo na kulewa kisha kuropoka kuhusu aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Fridah Kajala Masanja kwenye Instagram.

Mapema mwezi huu, Konde Boy alitishia kufunguka kuhusu utapeli wa Kajala baada ya kubugia chupa kadhaa za tembo na kulewa.

Siku ya Jumatano wiki iliyopita, mara baada ya mahojiano ya Kajala na wanahabari, Harmonize alitangaza kuwa yuko tayari kulewa na hata akaendelea kukata maji.

“Ohooo!!! Pombe zimeanza kuingia,” Harmonize alitangaza katika moja ya taarifa zake kwenye mtandao wa Instagram.

Katika sasisho lingine, alidokeza kuwa tayari alikuwa amelewa.

"Alooo nimelewa!!!"

Siku iliyofuata, Alhamisi, mwanamuziki huyo aliandika taarifa ndefu ambapo alimshambulia Kajala na kumtaka aache kugombana naye kwenye mitandao ya kijamii na badala yake atafute mwanaume wa kumuoa.