Harmonize na Rayvanny hatimaye wazika tofauti zao baada ya kuzozana muda mrefu

Mzozo wao ulitimbuka mwaka 2021 baada ya Rayvanny kudaiwa kuanika picha za uchi za Harmonize

Muhtasari

•Wawili hao wameanza kufuatiliana tena kwenye Instagram baada ya kuwa wamezuiana kwenye mtandao huo wa kijamii kwa muda mrefu.

•Haya yanajiri wiki chache tu baada ya wawili hao kutupiana cheche za maneno kwenye mitandao ya kijamii.

Rayvanny na Harmonize
Image: INSTAGRAM

Mastaa wawili wa Bongo, Harmonize na Rayvanny, wanadaiwa kutupilia mbali tofauti zao nyingi za muda mrefu.

Wasanii hao wawili ambao waliwahi kuwa chini ya usimamizi wa WCB hatimaye wameanza kufuatiliana tena kwenye Instagram baada ya kuwa wamezuiana kwenye mtandao huo wa kijamii kwa muda mrefu.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya wawili hao kutupiana cheche za maneno kwenye mitandao ya kijamii. Vita vya maneno baina yao vilianza baada ya Harmonize kuwashauri wasanii dhidi ya nyimbo za pombe.

"Wasanii punguzeni nyimbo za Pombe!! Msidhani hii nchi kila mtu ni mlevi😂 Hata tunaokunywanga Juma 3 Hatunywi tukisikia nyimbo za Pome kama unatonesha Kidonda!! Hasa Hasa January Hii," Harmonize aliandika.

Katika jibu lake, Rayvanny alibainisha kuwa mwenzake huyo wa zamani katika WCB hajawahi kutoa wimbo wa pombe uliovuma.

Rayvanny alibainisha kuwa yeye alihusika katika wimbo mkubwa wa Pombe wakati Harmonize akiwa bado anahangaika.

"Mandakiwe, Huo sio wimbo wako. Shukuru wa Kusini," alisema.

Mzozo kati ya mastaa hao wawili ulitimbuka mwaka 2021 baada ya Rayvanny kudaiwa kuanika picha za uchi za Harmonize. Wakati huo, Harmonize alikuwa akichumbiana na muigizaji wa filamu Bongo, Frida Kajala Masanja huku Rayvanny akitoka kimapenzi na binti yake wa pekee, Paula Paul.

Wakati vita hivyo vya mtandaoni vya hivi majuzi vikiendelea, Harmonize alimuuliza mwimbaji huyo mwenzake kwanini anamchukia sana. Bosi huyo wa Kondegang alichukua fursa hiyo kumkumbusha kuhusu mzozo wao wa hapo awali ambao ulisambaratisha mahusiano yake na Kajala mwaka wa 2021.

"Ulifanya kila mtu aone sehemu yangu ya siri, ulitaka nijiuwe na bado niko hapa. Usinichukie wenda Mungu ananiweka kwaajili yako uendelee kuwa inspired . Kuja kwa nyumba yangu nitakuonyesha jinsi ya kutengeneza pesa uweze kulipa label (WCB) ili uweze kutoka kabisa," Aliandika Harmonize.

Harmonize na Rayvanny waliwahi kuwa pamoja katika lebo ya WCB ambayo inasimamiwa na Diamond Platnumz. Wawili hao hata hivyo tayari wamegura lebo hiyo na kuanzisha lebo zao kivyao.