Harmonize adokeza mama yake alimuonya kuhusu kufunga ndoa na Kajala

"Mtu anayeitwa mzazi msikilize, hata asiyekuwa wako," Harmonize alisema.

Muhtasari

•Katika ufichuzi ambao alifanya kama ushauri, bosi huyo wa Konde Music Worldwide  aliwashauri watu kuwapa sikio wazazi wao kila siku.

• Harmonize alifichua kwamba hapo awali karibu aingie kwenye ndoa mbaya ambayo mzazi wake alikuwa amemuonya dhidi yake.

Kajala na Harmonize wakati mahaba yao yalikuwa yamenoga
Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amedokeza kuwa mama yake alimtahadharisha kuhusu aliyekuwa mpenzi wake.

Katika ufichuzi ambao alifanya kama ushauri, bosi huyo wa Konde Music Worldwide  aliwashauri watu kuwapa sikio wazazi wao kila siku..

Harmonize  alibainisha kwamba wazazi huwa na jicho maalum la kuwasaidia kuona mambo yaliyofichwa ndani ya mtu.

"Msikilize mama!! Awe ni mama yako mzazi au mama wa mwenzio, baba yako ama wa mwenzio.. wazazi wanakuwanga na jicho la mbali sana. Mzazi ni rahisi kugundua kila kitu. Inawezekana ukawa unajiona unajua kila kitu kumbe kuna jicho la mama. Akiangalia kitu au mtu anapata jibu sahihi kuliko wewe," alisema siku ya Alhamisi.

Mwimbaji huyo mahiri aliwasihi watu kutilia maanani pingamizi zinazowekwa na wazazi wao bila kujali jinsi zinavyochukiza.

Pia aliwataka watu kuwasikiliza wazazi wa wenzao hasa kuhusu masuala ya uhusiano bila kujali jinsi mahaba yalivyo mazito.

"Unaweza kuona kama kwamba huyu mama hanipendi akiwa mama wa mwenzio kumbe  huenda anajua kwamba mtoto wake hayupo tayari ila anakosa au anashindwa jinsi ya kukufanya uelewe maana upo kwenye dimbwi la mapenzi," alisema.

"Akiwa mzazi wako ni rahisi kukukataza hata kwa kutumia nguvu zote ila ukiwa umezama humuelewi," 

Wakati huo, alifichua kwamba hapo awali karibu aingie kwenye ndoa mbaya ambayo mzazi wake alikuwa amemuonya dhidi yake.

"Mtu anayeitwa mzazi msikilize hata asiyekuwa wako," alisema.

Staa huyo wa Bongo alitangaza kwamba atafanya ufichuzi zaidi kuhusu kilichofanyika mnamo siku ya wapendanao, Februari 14.

Pia alisisitiza kwamba kwa sasa hayuko kwenye mahusiano yoyote huku akionyesha kujivunia kwake kuwa single.

Kajala alitangaza kuhusu kuvunjika kwa mahusiano yake ya miezi kadhaa na Konde Boy mapema mwezi Desemba.

Ingawa hakuweka wazi kilichowatenganisha, alibainisha kuwa hakubeba kinyongo dhidi ya mwimbaji huyo licha ya mahusiano kugonga mwamba.

Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.

Mama huyo wa binti mmoja aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano kusambaratika.

Wawili hao walikuwa wamerudiana mapema mwaka jana baada ya kuwa wametengana kwa takriban mwaka mmoja.

Mahusiano yao ya kwanza yaliisha Aprili 2021 huku Harmonize akidaiwa kujaribu kumtongoza bintiye Kajala, Paula.