Ibraah wa Konde Gang afunguka aliyojifunza kwenye mahusiano ya Harmonize na Kajala

Ibraah aliyatakia kheri njema mahusiano ya mabosi hao wake wawili.

Muhtasari

•Ibraah alikiri kuwa ameweza kujifunza umuhimu wa ukakamavu katika mahusiano kutoka kwa wawili hao.

•Mapema mwaka huu Harmonize alitangaza kutengana kwake na Briana na kudai kuwa mojawapo ya sababu zilizochangia hatua hiyo ni kuwa moyo wake ulimtaka Kajala tu

Msanii Harmonize akimsherehekea mchumba wake Fridah Kajala Masanja
Msanii Harmonize akimsherehekea mchumba wake Fridah Kajala Masanja
Image: iNSTAGRAM//HARMONIZE

Msanii wa Konde Gang Ibraah ameyasherehekea mahusiano kati ya bosi wake Harmonize na muigizaji Kajala Masanja.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ibraah alikiri kuwa ameweza kujifunza umuhimu wa ukakamavu katika mahusiano kutoka kwa wawili hao.

"Ni watu wawili ambao wamepitia changamoto  nyingi lakini mwisho wa siku imekuwa ni mapenzi tu. Wao wanapendana," Ibraah alisema.

Staa huyo wa Bongo mwenye umri wa miaka 23 pia aliyatakia kheri njema mahusiano ya mabosi hao wake wawili.

"Mi naomba mwenyezi Mungu azidi kuwanyooshea, wafanikiwe zaidi na zaidi," Aliongeza.

Takriban miezi miwili imepita sasa tangu Konde Boy na Kajala kurudiana baada ya kutokuwa na uhusiano mzuri kwa mwaka mmoja.

Wasanii hao wa Bongo walitengana Aprili mwaka jana huku uvumi mwingi kuhusu sababu ya kutengana ukienea. Walikuwa wamechumbiana kwa kipindi cha miezi michache tu kabla ya kutengana.

Harmonize aliendelea kujitosa kwenye mahusiano mengine na mwanamitindo Briana Jai baada ya kutengana na Kajala.

Hata hivyo mapema mwaka huu bosi huyo wa Konde Music Wordwide alitangaza kutengana kwake na Briana na kudai kuwa mojawapo ya sababu zilizochangia hatua hiyo ni kuwa moyo wake ulimtaka Kajala tu.

"Kuhusu Briana sina Tatizo naye kabisa, yeye ni mtu mzuri ila hatuko pamoja, sababu moja  nilimwambia nimetengana na mtu bila kugomabana na nampenda sana sasa sina uhakika kama nimemove on lolote linaweza kutokea maana itakuwa ni kitendo kizalendo pia mimi kurudi nyumbani," Harmonize alitangaza kupitia Instagram mwezi Machi.

Mwishoni mwa mwezi Juni, Harmonize alimvisha Kajala pete ya uchumba na kutangaza mipango ya harusi.

Akitoa hotuba yake baada ya Kajala kukubali ombi la ndoa, Harmonize  alisimulia jinsi mama huyo wa binti mmoja alivyomkaribisha kwake wakati alipokuwa akipitia kipindi kigumu sana cha maisha yake.

"Umekuwepo kwa ajili yangu katika mambo mengi ambayo siwezi kueleza hivi sasa. Ni siri kati yangu na wewe na hata mara zingine umeniambia nisiseme hadharani. Kuna wakati nilikuwa napatia wakati mgumu hata ukanichukua, nikaishi nyumbani kwako na ni hivi majuzi. Sikuwa na nyumba au hata pa kulala... na hiyo imekuwa siri kati yangu na wewe na umeificha, hujai kuzungumzia mtu yeyote," Alisema.

Wachumba hao wameonekana kufurahia maisha pamoja baada ya kurudiana huku Harmonize hata akimfanya muigizaji huyo kuwa meneja wake.