Kunani? Huddah azua tetesi mpya za mahusiano na Jux baada ya kuthibitisha alitengana na Karen Bujulu

Alidokeza kuwa hamuachi mwimbaji huyo wa bongo kama maneno ya wimbo waliofanya mwaka wa 2022 yalivyosema.

Muhtasari

•Huddah amewasha moto mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kufufua kumbukumbu zake nzuri na mwimbaji wa Tanzania, Juma Jux.

•Wanamitandao wamevutiwa na posti hizo huku wengine wakifufua tetesi kuwa mastaa hao wawili wako kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Image: INSTAGRAM// HUDDAH MONROE

Mwanasosholaiti maarufu wa Kenya Huddah Monroe amewasha moto mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kufufua kumbukumbu zake nzuri na mwimbaji wa Tanzania, Juma Jux.

Siku ya Jumamosi, mwanasosholaiti huyo ambaye anaishi kwa kiasi nchini Kenya na Dubai alichapisha picha kadhaa za kumbukumbu zinazoonyesha nyakati za kimapenzi na Jux.

Picha nyingi alizochapisha zilipigwa wakati wa kurekodi video ya wimbo wa staa huyo wa bongo ‘Simuachi.’

"Ulichosema wimbo huo" Huddah alisema chini ya moja ya picha hizo.

Hii huenda lilikuwa kudokeza kuwa hamuachi mwimbaji huyo wa bongo kama maneno ya wimbo waliofanya mwaka wa 2022 yalivyosema.

Wanamitandao wamevutiwa sana na posti hizo huku wengine wakifufua tetesi kuwa mastaa hao wawili wako kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Hatua hii inajiri siku chache tu baada ya Juma Jux kuthibitisha kuwa hana uhusiano tena na mrembo wa Tanzania Karen Bujulu.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Lily Ommy, Jux alifichua kuwa aliachana na Bi Bujulu takriban miezi mitatu iliyopita.

Aliendelea kuzungumzia madai kuwa uhusiano wake ulishindikana baada ya Ommy Dimpoz kuingia kati ya muungano wao.

Mapema taarifa zilisambaa zikieleza kuwa Ommy ambaye ni rafiki mkubwa wa Juma alikuwa akimtongoza Karen, kitu ambacho kilihatarisha uhusiano wake.

Hata hivyo, mwimbaji huyo wa Enjoy alishindwa kueleza iwapo madai hayo ni ya kweli au la kusema pia alisikia madai hayo kwenye mitandao ya kijamii.

“Ni kweli mimi na Karen hatuko pamoja tena. Imekuwa kama miezi mitatu hadi minne sasa,” Juma alisema.

Mapema mwaka wa 2022, Huddah na Jux waliwakanganya mashabiki wao kuhusu uhusiano wao baada ya kuonekana pamoja mara kwa mara na hata kufanya mambo mbalimbali ambayo yalidokeza wanachumbiana. Wawili hao walionekana wakijivinjari pamoja, wakikumbatiana na hata kupigana busu hadharani.

Katika video moja iliyowaonyesha wakiwa wamebarizi nyumbani kwake Jux, wawili hao hawakuogopa kubusu mbele ya kamera na kuambiana maneno matamu ya kimapenzi. 

"Mimi na mpenzi wangu tumetulia tu.. sijui, ningependa kuwa kitandani na wewe," Huddah alisikika akimwambia Jux.

Haya yalitokea siku chache tu baada ya staa huyo wa Bongo kumshirikisha Huddah katika video ya kibao chake 'Simuachi.'