Lukamba afunguka kuhusu maisha baada ya kutengana na Diamond, sababu ya kukonda

Mpiga picha huyo alikiri kuwa alikula bata ya kutosha wakati akifanya kazi na Diamond.

Muhtasari

•Lukamba alitamatisha uhusiano wake na Diamond  takriban miezi minne iliyopita na kuanzisha kampuni yake ya Imagix Media.

•Alikiri kwamba majukumu mengi ambayo amekuwa nayo ndiyo yamepunguza mwili wake kwa kiasi kikubwa.

katika picha ya maktaba.
Lukamba na Diamond katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Mpiga picha rasmi wa zamani wa Diamond Platnumz,  Ashraf Haji Lukamba amefunguka kuhusu maisha yake baada ya kugura WCB.

Lukamba alitamatisha uhusiano wake na Diamond  takriban miezi minne iliyopita na kuanzisha kampuni yake ya Imagix Media.

Msanii huyo amejitokeza na kuweka wazi kuwa maisha yake yanaendelea vizuri licha ya sasa kulazimika kujisimama mwenyewe.

"Sasa hivi sifocus sana kwenye bata. Naangazia kujijenga mimi mwenyewe," alisema katika mahojiano na Wasafi Media.

Alikiri kuwa alikula bata ya kutosha wakati akifanya kazi na Diamond na hatazamii nyuma kwenye maisha hayo kwa sasa.

"Muda mwingi sasa natumia kuweka maisha yangu yawe sawa.Kusema kweli hakuna chochote ambacho namiss," alisema.

Mpiga picha huyo ambaye kwa sasa amejitosa kwenye muziki alifichua kwamba amekuwa na majukumu mengi tangu kuondoka WCB.

Alikiri kwamba majukumu mengi ambayo amekuwa nayo ndiyo yamepunguza mwili wake kwa kiasi kikubwa.

"Muda mwingi nafanya kazi. Sina muda wa kupumzika. Sasa ndio naelewa kwa nini Simba (Diamond)  alikuwa anapungua. vitu ni vingi sana," alisema.

Aliongeza, "Sasa hivi natengeneza himaya yangu. Kuna vitu vingi lazima nizisimamie mwenyewe. Lazima niwe bize."

Lukamba alianza kujitenga na bosi wa Wasafi mwishoni mwa mwaka jana kabla ya kutengana rasmi Juni mwaka huu.

Mwezi Agosti alizindua kampuni yake kwa jina Imagix Media kama ishara ya mwanzo mpya baada ya kugura WCB. Amefichua alitumia takriban millioni mia mbili za Tanzania (Ksh10M) kuanzisha kampuni hiyo.

"Ndio maana nakonda. Ndio maana hata nashindwa kubadilisha gari," alisema.

Pia anamiliki programu ya video ya Lukashnet ambayo anadai alitumia mamilioni ya pesa kuanzisha.

Katika mahojiano, Lukamba pia alichukua fursa kuwakashifu wakosoaji  wa muziki wake na kueleza matumaini yake ya kuwa msanii mkubwa katika siku za usoni. Alisema kuwa anafanya muziki kwa kasi yake na haigi mwanamuziki mwingine yule.