"Mengine zungumza na Kajala!" Harmonize afichua ubosi wa mchumba wake

Kajala alianza kazi yake katika Konde Gang rasmi mapema mwezi uliopita.

Muhtasari

•Harmonize amebainisha kuwa kazi yake ni kutumbuiza popote anapoalikwa huku mchumba wake Kajala  akiongoza mazungumzo yote  kuhusiana na shoo anazofanya.

•Kando na kuwa mchumba wa Harmonize, Kajala pia ni mkurugenzi mtendaji wa timu ya mameneja wa Konde Gang.

Msanii Harmonize akimsherehekea mchumba wake Fridah Kajala Masanja
Msanii Harmonize akimsherehekea mchumba wake Fridah Kajala Masanja
Image: iNSTAGRAM//HARMONIZE

Staa wa Bongo Harmonize ameweka wazi kwa waandaaji tamasha kwamba huwa hahusiki katika mazungumzo yoyote ya kibiashara.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bosi huyo wa Konde Gang amebainisha kuwa kazi yake ni kutumbuiza popote anapoalikwa huku mchumba wake Kajala Masanja akiongoza mazungumzo yote  kuhusiana na shoo anazofanya.

"Ninaimba na kutumbuiza tu. Mengine, zungumza naye (Kajala), usipoteze muda wako isipokuwa kama unataka kuvuta sigara nami," Harmonize alisema kupitia Instastori zake.

Msanii  huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha inayomuonyesha akiwa ameandamana na Kajala wakati wa ziara yake ya hivi majuzi nchini Burundi

Kando na kuwa mchumba wa Harmonize, Kajala pia ni mkurugenzi mtendaji wa timu ya mameneja wa Konde Gang.

Mwezi Juni Harmonize alimuongeza mchumba wake kwenye timu yake ya wasimamizi, miezi michache tu baada yao kurudiana. Choppa TZ, mmoja wa mameneja wake ndiye aliyetangaza habari za uteuzi wa Kajala huku akimkaribisha katika timu yao.

"Niruhusu nimkaribishe katika timu ya usimamizi mkurugenzi na meneja mpya Frida Kajala. Nimefurahi kufanya kazi na wewe shem," Choppa alitangaza kupitia Instagram.

Muigizaji huyo alianza kazi yake rasmi mapema mwezi uliopita, habari ambazo Harmonize aliwatangazia mashabiki wake.

"Ukiona nang'aa ujue ni kazi ya mpenzi  wangu @kajalafrida. Anaanza kazi yake rasmi leo," Konde Boy alisema mnamo Julai 7.

Katika Konde Gang, Kajala anashirikiana na mameneja wengine kama vile Chopa, Mjerumani na Jose Wamipango.