"Naweza rogwa bure!" Samidoh afunguka ukweli kuhusu kununuliwa pombe ya 420k na Karen Nyamu

Samidoh amedokeza kwamba haikuwa kweli na ilikuwa ni maigizo tu ya mitandao ya kijamii.

Muhtasari

•Samidoh aliwataka wanamitandao kutochukulia kila kitu kwa uzito akidokeza kuwa pombe ya bei ghali inayodaiwa alinunuliwa na mzazi mwenzake si ya kweli.

•“Hehe hizo ni vipindiree vya mitandao ya kijamii usichukulie serious sana. Naweza rogwa bure,” Samidoh alijibu.

Karen Nyamu na Samidoh
Image: HISANI

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh amedokeza kuwa mpenzi wake Karen Nyamu alidanganya kuhusu kumnunulia pombe ya bei ghali.

Mnamo siku ya kuwasherehekea kina baba mwezi uliopita, seneta huyo wa UDA alishiriki video yake akiwa katika duka la kuuza vileo ambapo alidai alinunua pombe ya Ksh 420,000 kama zawadi kwa baba wa watoto wake wawili wadogo.

Samidoh hata hivyo amedokeza kwamba haikuwa kweli na ilikuwa ni maigizo tu ya mitandao ya kijamii.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook siku ya Jumapili jioni, aliandika, “Waweru Uyu na Kajei Salim kumbe maswali zenu nyingi za kifala ni za Captain Morgan. Kwa sababu bia haiulizi maswali ya kipuuzi buana. Niko Muthiga kujeni mnipige.”

Mwimbaji huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa ameshikilia kikombe ambacho kilionekana kuwa na bia ndani yake.

Mmoja wa mashabiki wake alitaka kujua iwapo pombe aliyokuwa ameshika ni ile ambayo Karen Nyamu alidaiwa kumnunulia.

“Thamweri, hiyo ni ile ya 420k. Bado iko kwa friji,” Princess Priscah Wambui alitoa maoni chini ya chapisho la mwimbaji huyo.

Katika jibu lake, Samidoh aliwataka wanamitandao kutochukulia kila kitu kwa uzito akidokeza kwamba pombe ya bei ghali inayodaiwa alinunuliwa na mzazi mwenzake si ya kweli.

“Hehe hizo ni vipindiree vya mitandao ya kijamii usichukulie serious sana. Naweza rogwa bure,” alijibu.

Mwezi uliopita, Karen Nyamu alidai kwamba alinunua pombe yenye thamani ya Sh420,000 kwa ajili ya baba huyo wa watoto wake.

Katika video hiyo iliyosambaa mitandaoni, Nyamu alionekana akiingia kwenye duka la kuuza vileo na kuagiza pombe ya bei ghali zaidi waliyokuwa nayo dukani.

"Nimekuja kununulia mbabaz pombe ya father's day. Nataka ile ya dooh mob kabisaa kwa mbabaz.. Ghali zaidi kabisaa, nataka kubuiya mbabaz," Karen Nyamu alimwambia mhudumu wa duka hilo huku akizunguka zunguka kwenye biashara hiyo kubwa kwa furaha akitazama huku na kule.

Mhudumu huyo wa duka la vileo aliandamana naye akimuonyesha chupa tofauti za kuanzia 210k hadi 420K.

Karen alisikika akitania kwamba chupa ya pombe ya 420,000 ilikuwa sawa na kununua Toyota Vitz.

Kisha akaendelea kuchukua chupa ya pombe ya Remy Martin ya 700ml Louis XIII kwa ajili ya mubabaz wake. Mhudumu wa duka hilo kwa furaha alimwonyesha Karen jinsi ya kufungua sanduku la vileo huku wakizungumza.

Bila kusitasita, Karen alionekana kuendelea kulipia chupa hiyo ya pombe hiyo kwa kutumia kadi yake ya mkopo, kisha akaendelea kupiga picha.

Ili kuthibitisha ununuzi wa pombe hiyo, mwanasiasa huyo alionyesha screenshot ya malipo kwenye Instastori zake.