“Nilimhitaji zaidi!” Karen Nyamu athibitisha maelezo ya Edday Nderitu kuhusu kwa nini alimuacha Samidoh

Katika jibu lake, mwanasiasa huyo aliweka wazi kuwa alimhitaji mpenzi huyo wake zaidi na akakiri furaha kubwa aliyo nayo kuwa naye.

Muhtasari

•Mtumiaji mmoja wa Facebook alishambulia seneta huyo kwa madai kuwa mwanaume aliye naye si wake bali ni wa mtu mwingine.

•Mwezi Julai, Bi Nderitu aliweka wazi kuwa alimuacha mumewe ili kuwa na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alitoa jibu la utani baada ya kushutumiwa kwa kuwa kwenye mahusiano na mpenzi wa mtu mwingine.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu alikuwa ameweka posti akiwashauri watu kuhusu nini cha kufanya wanapowapeza wapenzi wao.

“Ukimiss mpermanent wako shikilia pillow. Sitawafunza kila kitu pia nyinyi,” Karen Nyamu  alisema kwenye Facebook Jumatano asubuhi.

Nyamu aliambatanisha maelezo yake na picha yake ndani ya ndege huku akiwa ameshikilia mto mikononi mwake. Katika sehemu ya maoni, kama inavyotarajiwa, watumiaji wa mtandao walikuwa na maoni mseto ya kutoa.

Mtumiaji mmoja wa Facebook alishambulia seneta huyo kwa madai kuwa mwanaume aliye naye si wake bali ni wa mtu mwingine.

"Wako ni M-kopa wa wenyewe," Sonnie Mwangi Mso alisema.

Katika jibu lake, mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi aliweka wazi kuwa alimhitaji mpenziwe zaidi na akakiri furaha kubwa aliyo nayo kuwa naye.

"Nilimhitaji zaidi na maisha ni ya haki," Karen Nyamu alijibu.

Hii ilionekana kuthibitisha kauli ya mke wa kwanza wa Samidoh, Edday Nderitu mapema mwaka huu kwamba alimuacha mwimbaji huyo kuwa na mtu ambaye alimuhitaji zaidi.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Mwezi Julai, Bi Nderitu aliweka wazi kuwa alimuacha mumewe ili kuwa na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."

Edday alisema haya baada ya seneta Nyamu kudai kuwa Samidoh na Edday Nderitu bado wako katika uhusiano mzuri na huwa wanazungumza.

Katika mahojiano na na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, seneta Nyamu alifichua kuwa Edday ambaye kwa sasa anafurahia wakati na familia yake nchini Marekani bado huwa anawasiliana na Samidoh na akadai kwamba hawezi kwenda popote kwani muungano wao hauwezi kuvunjika kwa urahisi.

“Mambo mnayoyaona kwenye mitandao ya kijamii mtashangaa sana, kuna baadhi ya miungano imetoka mbali sana. Labda hajui kwamba haendi popote, lakini najua kwa sababu miungano mingine si rahisi kukatika,” alisema.

Nyamu alidokeza kuwa mpenzi wake Samidoh na mkewe wa kwanza wamechukua mapumziko lakini bado wako katika uhusiano mzuri.

“Huwa naskia wakiongea, wako sawa sio vile mnafikiria. Hata watoto wanaongea naye kupitia simu yake. Kwa ground hakutawahi haribika,” alisema.

Seneta huyo alisisitiza kuwa yeye si mharibifu na akadokeza kuwa kuna mambo makubwa yatajidhihirisha katika siku zijazo.