Samidoh ajibu kwa ukali baada ya kuagizwa kujiuzulu kutoka Polisi kuangazia ziara za muziki

Mwaka jana, Samidoh alisema hajapata sababu ya kuacha kazi ya kulinda usalama licha ya mafanikio yake katika tasnia ya muziki.

Muhtasari

•Shabiki alimtaka mwimbaji huyo kujiuzulu kutoka kwa huduma ya polisi na kuacha nafasi hiyo kwa Wakenya wengine wenye mahitaji kujaza.

•Katika majibu yake, Samidoh alionekana kutotiwa wasiwasi na agizo hilo.

Samidoh katika sare ya polisi
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alijibu kwa ukali baada ya shabiki kumtaka ajiuzulu kutoka kwa Huduma ya Polisi ya Kenya na kuangazia ziara zake za muziki.

Chini ya moja ya chapisho la mwanamuziki huyo kwenye Facebook, shabiki alidai kuwa serikali inaendelea kumlipa ilhali yeye ni mtalii zaidi kuliko afisa wa polisi.

Kutokana na ziara zake nyingi za muziki duniani, mtumiaji huyo wa Facebook aliyejitambulisha kama Macharia Mash alimtaka mwimbaji huyo kujiuzulu kutoka kwa huduma ya polisi na kuacha nafasi hiyo kwa Wakenya wengine wenye mahitaji kujaza.

“Na serikali inakulipa kama polisi na we ni more than a tourist ,si uresign tu uachie needy kenyans hio nafasi ya polisi juu hautaki kutulinda.....ata mtalii hawatembeagi vile unatembea baana,” shabiki alitoa maoni.

Katika majibu yake, Samidoh alionekana kutotiwa wasiwasi na agizo la mtumiaji huyo wa Facebook.

“Sasa unataka kulia?” alijibu.

Mwimbaji huyo wa Mugithi kwa sasa yuko jijini Melbourne, Australia ambako amekuwa akiwaburudisha mashabiki wake katika maeneo mbalimbali ya burudani. Ziara ya muziki ya Australia inakuja wiki chache tu baada ya kutumbuiza nchini Ujerumani na Dubai.

Image: FACEBOOK/// SAMIDOH

Mwaka jana, Samidoh ambaye kando na kuwa mwanamuziki pia ni afisa wa Polisi wa Utawala alisema hajapata sababu ya kuacha kazi ya kulinda usalama licha ya mafanikio yake katika tasnia ya muziki. Mara nyingi yeye hushiriki picha na video zake akitumbuiza katika sehemu mbalimbali za dunia lakini si akitoa huduma za afisa wa polisi.

"Ninafanya kazi siku za wiki na inapohitajika pamoja na kipindi cha wikendi huwa nafanya muziki wangu, kama talanta nyingine yoyote katika huduma ya polisi," alisema katika mahojiana na Word Is.

Msanii huyo alisema alijitahidi sana kupata kazi hiyo.

"Umewahi kwenda kwenye zoezi la kuajiri polisi na kuona watu wasio na mashati wakichukuliwa kupitia shughuli mbalimbali?" alisema.

"Kuacha kazi uliyotafuta chini ya mazingira hayo ni uchungu sana."