Pritty Vishy atambulisha mpenzi mpya baada ya Stivo kutangaza harusi na mchumba wake (+picha)

Vishy alimtambulisha mpenzi wake mpya kama "My Lord."

Muhtasari

•Siku ya Jumatano, Vishy alionyesha picha ya mwanaume ambaye alidokeza kuwa ni mpenzi wake mpya.

•Haya yanajiri siku chache baada ya aliyekuwa mpenzi wake, Stivo Simple Boy kudokeza kufanya harusi na mchumba wake.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Mtumbuizaji Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amedokeza kuwa amezama tena kwenye dimbwi la mahaba, takriban mwaka mmoja baada ya mahusiano yake na mwimbaji Stivo Simple Boy kugonga ukuta.

Siku ya Jumatano, Vishy alionyesha picha ya mwanaume ambaye alidokeza kuwa ni mpenzi wake mpya.

"Ananifanya nichizi," aliandika chini ya picha hiyo.

Pia alionyesha picha nyingine ya sehemu ya uso wa mwanaume huyo na kuendelea kudokeza mahusiano naye.

"Nimeskia wanafaa kuitwa My Lord si babe 🤣🤣🤣🤣 Ok, My Lord," aliandika kwenye picha hiyo na kuambatanisha na emoji za uso wenye makopakopa ya mapenzi.

Kwenye picha, ndevu kubwa za mwanaume huyo pekee zilinionekana kwani alificha sura kwa emoji ya mapenzi.

Haya yanajiri siku chache baada ya aliyekuwa mpenzi wake, Stivo Simple Boy kudokeza kufanya harusi na mchumba wake.

Mapema wiki hii, rapa huyo alichapisha picha ya suti na kuwaarifu mashabiki wake kwamba yuko tayari kuaga maisha ya ukapera. Pia alidokeza kuwa mchumba wake asiyejulikana anatokea kaunti ya Taita Taveta.

Mapema mapema fundi mtaalam tunampata alafu wangapi mnanipeleka Taveta naaga ukapera," alisema kwenye Instagram.

Siku moja kabla ya taarifa hiyo, mwanamuziki huyo alimtambulisha mchumba wake kwenye mitandao ya kijamii.

Stivo alichapisha picha nzuri iliyomuonyesha akiwa na mwanadada huyo na kuambatanisha na makopakopa ya mapenzi.

"Utam Utam vacation twende wapi? @zenahsimple😘😍 Katoto kamirigado nyataveta," aliandika chini ya picha hiyo.

Mwimbaji huyo alimtambulisha mke wake halisi hadharani wakati wa hafla ya mazishi ya babake mnamo Februari 11.

Stivo alikuwa akitoa hotuba yake alipomtambulisha mwenzi wake wa maisha asiyejulikana na wengi, Grace Atieno.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.

Baada ya kupokea kipaza sauti, Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina ni Grace Atieno. Nimeoleka kwa Bwana Stephen Otieno. Naskia vibaya kumpoteza mtu mwenye alikuwa akinitoa kila wakati..." Grace alisema kabla ya kuzidiwa na hisia na kuangua kilio.

Stivo aliachana na mpenzi wake wa muda mrefu Pritty Vishy mapema mwaka jana, miezi michache tu baada ya uhusiano wao kujulikana hadharani.

Wawili hao hata hivyo ilidaiwa hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani Stivo alidaiwa kutaka kusubiri ndoa kabla ya kushiriki tendo la ndoa na mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21.