"Usivunje ndoa yangu!" Stivo Simple Boy amlilia Pritty Vishy baada ya kumpost Valentine's

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Stivo Simple Boy kumtambulisha mkewe halisi.

Muhtasari

•Vishy alichapisha picha inayomwonyesha Simple Boy akimkabidhi maua nyekundu ya waridi akiwa ameketi kwenye kiti cheupe.

•"Usivunje ndoa yangu tafadhali. Mi niko welo welo nalishwa mapocho pocho uku siko soko niache tu," alimjibu Vishy.

Stivo Simple Boy na Pritty Vishy
Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Mtumbuizaji Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amesherehekea Siku ya Wapendanao kwa njia maalum kwa kuchapisha  picha  ya maktaba inayomuonyesha akiwa na mwanamuziki Stivo Simple Boy.

Siku ya Jumanne asubuhi, kipusa huyo mwenye umri wa miaka 21 alichapisha picha inayomwonyesha Simple Boy akimkabidhi maua nyekundu ya waridi akiwa ameketi kwenye kiti cheupe. Pichani, wapenzi hao wa zamani walikuwa wamevaa nguo nyeupe na walionekana wenye furaha pamoja.

"Kwa mashemeji wetu wa mitandaoni ata nyinyi mnaona ni Valentines❤❤," aliandika chini ya picha hiyo aliyopakia Instagram.

Aliongeza, "Anyway, kheri ya siku ya wapendanao jaherana🤣🤣🤣,"

Stivo ambaye alionyesha wazi kuwa hakupendezwa na chapisho hilo alionya mpenzi huyo dhidi ya kujaribu kuvunja ndoa yake.

Katika jibu lake, mwimbaji huyo wa 'Mihadarati' alimfahamisha Pritty Vishy kuwa yuko kwenye uhusiano mzuri na wenye furaha.

"Usivunje ndoa yangu tafadhali. Mi niko welo welo nalishwa mapocho pocho uku siko soko niache tu," alimjibu Vishy.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Stivo Simple Boy kumtambulisha mkewe halisi hadharani kwa mara ya kwanza.

Stivo alikuwa akitoa hotuba kwenye mazishi ya baba yake Anthony Adera siku ya  Jumamosi wakati alipomtambulisha mwenzi wake wa maisha, Grace Atieno.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.

Baada ya kupokea kipaza sauti, Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina ni Grace Atieno. Nimeoleka kwa Bwana Stephen Otieno. Naskia vibaya kumpoteza mtu mwenye alikuwa akinitoa kila wakati..." Grace alisema kabla ya kuzidiwa na hisia na kuangua kilio.

Baadaye, Pritty Vishy alionyesha kwamba haamini  mpenzi huyo wake wa zamani yuko kwenye ndoa halisi na mwanamke aliyemtambulisha kama mke wake wakati wa mazishi ya marehemu baba yake.

Vishy alikicheka  kitendo cha mpenzi huyo wake wa zamani kumtambulisha mwanamke mwingine kama mke wake.

Akizungumza kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, kipusa huyo mwenye umri wa miaka 21 alibainisha kuwa ni sharti hafla ya harusi ifanyike ili mwanamke kutambuliwa kama mke wa mtu.

"Mimi ndoa najua ni lazima kukuwe na harusi. Kama si hivyo hiyo ni 'kuja tukae' na hiyo sio ndoa," alisema.

Vishy alikuwa akimjibu shabiki aliyetaka kujua jibu lake kufuatia hatua ya Stivo kumtambulisha mke wake.

Wakati huo huo, pia aliweka wazi kuwa kuolewa haijawahi kuwa katika orodha ya matakwa yake maishani.