Stivo Simple Boy amtambulisha mke wake asiyejulikana kwenye mazishi ya babake

"Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema

Muhtasari

•Stivo alikuwa akitoa hotuba yake alipomtambulisha mwenzi wake wa maisha asiyejulikana na wengi, Grace Atieno.

•Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

amemtambulisha mke wake Grace Atieno
Stivo Simple Boy amemtambulisha mke wake Grace Atieno
Image: HISANI

Rapa mashuhuri Stephen Otieno Odera almaarufu Stivo Simple Boy hatimaye alimtambulisha mke wake halisi hadharani wakati wa hafla ya babake siku ya Jumamosi.

Stivo alikuwa akitoa hotuba yake alipomtambulisha mwenzi wake wa maisha asiyejulikana na wengi, Grace Atieno.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.

Baada ya kupokea kipaza sauti, Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina ni Grace Atieno. Nimeoleka kwa Bwana Stephen Otieno. Naskia vibaya kumpoteza mtu mwenye alikuwa akinitoa kila wakati..." Grace alisema kabla ya kuzidiwa na hisia na kuangua kilio.

Babake Stivo, Bw Anthony Odera alizikwa siku ya Jumamosi nyumbani kwake katika eneo la Oyugis, kaunti ya Homa Bay.

Marehemu aliaga dunia mwezi uliopita kukumbwa na ugonjwa usiothibitishwa.

Huku akitangaza kifo cha babake mwezi jana, msanii huyo kutoka Kibra alidokeza kwamba inauma sana moyoni kumpoteza mzazi huyo wake na kuwaomba mashabiki kuendelea kusimama naye.

"Ningependa kuwaambia mashabiki wangu kwamba nimepata msiba ya kupoteza babangu mzazi Anthony Adera. Ni uchungu sana kupoteza mzazi ila naomba mniombee na mnisapoti kwa huu wakati mgumu," alisema.

Stivo aliwataka mashabiki wake kumuombea na kumpa nguvu huku akiendelea kumuomboleza baba yake mpendwa.

Maelezo machache yanajulikana hadharani kuhusu mke wa mwimbaji huyo wa nyimbo za kufoka, Grace Atieno.

Stivo aliachana na mpenzi wake wa muda mrefu Pritty Vishy mapema mwaka jana, miezi michache tu baada ya uhusiano wao kujulikana hadharani.

Wawili hao hata hivyo ilidaiwa hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani Stivo alidaiwa kutaka kusubiri ndoa kabla ya kushiriki tendo la ndoa na mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21.