Stivo afunguka jinsi alivyokutana na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy

Muhtasari

•Simple Boy ameweka wazi kuwa yeye ndiye aliyechukua hatua ya kumchumbia mpenzi huyo wake wa zamani.

•Mwanamuziki huyo alisema kuwa alimpenda sana kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 ila akakosa subira.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Mwanamuziki Stivo Simple Boy amefichua kwamba alikutana na Pritty Vishy  akiwa bado mwanafunzi wa darasa la nane.

Simple Boy ameweka wazi kuwa yeye ndiye aliyechukua hatua ya kumchumbia mpenzi huyo wake wa zamani.

Akiwa kwenye mahojiano na Oga Obinna, Stivo alisema walikubaliana na Vishy amalize masomo yake hadi shule ya upili ili waweze kufunga ndoa.

"Tulikutana kitambo akiwa darasa la nane. Nilimwambia akimaliza shule aende shule ya upili bado nitakuwa nimemsubiri," Stivo alisema.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa alimpenda sana kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 ila akakosa subira.

Alidai kuwa mpenzi huyo wake wa zamani hakuwa mwaminifu na aliwahi kutoka kimapenzi na wanaume zaidi ya 50 katika kipindi cha mahusiano yao.

"Mimi nilinyamazia tu. Nilikuwa nikimwambia  kama ananipenda cha kweli awachane na hayo mambo yake. Nilimwambia akuwe na mtu mmoja ili tufunge ndoa. Lakini haeleweki jameni," Alisema.

Stivo aliweka wazi kuwa hana mpango wowote wa kuwahi kurudiana na Vishy huku akidai kuwa alitenda makosa mengi kiasi cha kutostahili msamaha.

Mwanamuziki huyo pia alifichua kuwa alikatiza masomo yake katika darasa la nane kisha akazamia jijini Nairobi kutafuta riziki.

Alianza kuvuma mwaka wa 2019 baada ya kuachia kibao 'Mihadarati' ambacho kiliwasisimua sana Wakenya.