Stivo Simple Boy afichua sifa ambazo anaangalia kwa mke

Muhtasari

•Stivo alibainisha kuwa aliyekuwa mpenzi wake, Pritty Vishy hakuwa mwanamke sahihi kwake kuoa. 

•Alifichua kuwa kuna wanadada wengi ambao wamekuwa wakimtongoza hasa kupitita mitandao ya kijamii.

Image: INSTAGRAM// STIVO SIMPLE BOY

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Kibra Stivo Simple Boy amesema bado anasubiri mtu bora zaidi wa kuingia kwenye ndoa naye.

Akiwa kwenye mahojiano na Oga Obinna, Stivo pia alidokeza kuwa atakuwa tayari kushiriki tendo la ndoa pindi tu atakapopata mwanamke sahihi wa kuoa.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 31 alibainisha kuwa aliyekuwa mpenzi wake, Pritty Vishy hakuwa mwanamke sahihi kwake kuoa.

"Tulikutana naye kitambo akiwa darasa la nane. Nilimwambia amalize shule kisha aende shule ya upili ningemsubiri. Wasichana hawana uvumilivu.. Nilikuwa najua mambo yake lakini ningependa ashikilie mtu mmoja. Yeye si wa mtu mmoja. Najua wanaume zaidi ya 50 ambao amekuwa nao," Simple Boy alisema.

Stivo alisema alijaribu sana kumsihi mpenzi huyo wake wa zamani akubali kubadilisha mienendo yake ili waweze kufunga ndoa  lakini hakufua dafu. Alidai kuwa Vishy alikosea sana na akasema hatakuwa tayari kukubali ombi lake la msamaha ikiwa itatokea achukue hatua hiyo.

Mwanamuziki huyo alisema bado anatafuta mwanamke bora ambaye atatimiza mahitaji yake yote kwa mke.

"Kwanza lazima akuwa Mcha Mungu. Lazima akuwe mnyenyekevu, aniheshimu na pia mimi nimheshimu. Kama nimefanya kosa aniambie na pia akifanya kosa akubali," Alisema.

Stivo alifichua kuwa kuna wanadada wengi ambao wamekuwa wakimtongoza hasa kupitita mitandao ya kijamii.

Alisema hata hivyo amekuwa akiwapuuzilia kwa kuwa ni ngumu kubainisha mwanamke aliye na hisia za kweli.