(+Video) Baraka nyingine! Bahati na Diana Marua watangaza ujauzito wa mtoto wa tatu

Walitangaza habari za ujauzito kupitia wimbo 'Nakulombotov' ambao walishirikiana.

Muhtasari

•Diana aliufichua ujauzito wake mkubwa katika video ya wimbo huo 'Nakulombotov' ambao alishirikiana na mumewe.

•Wawili hao pia walimhakishia mtoto wao kuhusu upendo wao mkubwa kwake na kumtakia baraka tele maishani.

Wanandoa Bahati na Diana Marua wanatarajia mtoto wao wa tatu pamoja.

Wawili hao walitangaza habari za ujauzito kupitia wimbo ambao walipakia kwenye Youtube Ijumaa mwendo wa adhuhuri.

Diana aliufichua ujauzito wake mkubwa katika video ya wimbo huo 'Nakulombotov' ambao alishirikiana na mumewe.

"Baraka nyingine..  Asante Mungu," Diana aliandika chini ya video ya wimbo huo iliyopakiwa kwenye akaunti yake ya YouTube.

Katika wimbo huo wa dakika tatu wanandoa hao walitoa ahadi kemkem na ushauri kwa mtoto wao ambaye hajazaliwa.

Wawili hao pia walimhakishia mtoto wao kuhusu upendo wao mkubwa kwake na kumtakia baraka tele maishani.

"Nakutakia baraka, nakutakia fanaka,

Nakutolea sadaka, nyota yako itawaka,

Utamkia neema isiyokuwa na mipaka.

Maisha mazuri, uishi mamiaka.

Magonjwa na mikosi na zikae mbali,

Malaika wakulinde dhidi ya ajali.

Hekima ikutawale kama serikali,

Nasi tunakusubiri kama fainali,"  Diana alisema katika kipande cha wimbo huo.

Diana pia alimfahamisha mtoto wake kuhusu jinsi  dunia ilivyo huku akimueleza kuwa kwa kawaida mambo sio rahisi.

Tangazo lao linajiri siku chache tu baada ya Bahati kudai kwamba wangetembelea kituo cha afya kubaini ikiwa mkewe ni mjamzito.

Wawili hao wamekuwa wakidinda kujibu tetesi nyingi za ujauzito ambazo zimekuwa zikienezwa kwa muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii.

Kwani kuna watu wanakuwanga bedroom yetu. Ni maoni tu. Kusema kweli wamekisia sana, tutaenda hospitali tupime. Haiwezi kuwa watu wanakisia na sijui," Bahati alijibu mapema mwezi huu wakati alipohojiwa kuhusu ujauzito.

Diana na Bahati tayari wana watoto wawili pamoja. Wanandoa hao walibarikiwa na mtoto wa kwanza pamoja, Heaven Bahati, mwezi Februari 2018.

Mnamo Agosti 14, 2019 wanandoa hao walikaribisha mtoto wao wawili pamoja, Majesty Bahati.

Isitoshe, wawili hao pia wameadopt mvulana mmoja anayetambulika kama Morgan Bahati. Bahati alimchukua Morgan kama mtoto wake takriban miaka nane iliyopita.

Bahati pia ana mtoto mwingine wa kike, Mueni Bahati, ambaye alipata na aliyekuwa mpenzi wake kabla ya Diana, Yvette Obura.