Guardian Angel amimina mapenzi kwa mkewe Esther Musila anapoadhimisha hatua maalum

Guardian Angel alimtaja mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 kuwa mpenzi wake na kubainisha kuwa yeye ni baraka kubwa.

Muhtasari

•Musila alisherehekea kazi yake ya utumishi wa Umma wa Kimataifa kwa zaidi ya miongo miwili na ujumbe mzuri kwake ambapo alipongeza juhudi zake mwenyewe za kuhudumia watu.

•Guardian Angel ni miongoni mwa Wakenya ambao wamejitokeza kumpongeza kwa hatua hiyo kubwa ya kikazi aliyopiga.

Esther Musila na mume wake Guardian Angel
Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Siku ya leo, Agosti 7, mke wa mwimbaji wa nyimbo za Injili Guardian Angel, Bi Esther Musila anaadhimisha miaka 22 tangu aanze kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa (UN).

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alisherehekea kazi yake ya utumishi wa Umma wa Kimataifa kwa zaidi ya miongo miwili na ujumbe mzuri kwake ambapo alipongeza juhudi zake mwenyewe za kuhudumia watu.

"Leo ninaadhimisha miaka 22 ya utumishi kama Mtumishi wa Umma wa Kimataifa. Ninaomba kwa njia yangu ndogo, nimetoa mchango unaostahili katika kutumikia walimwengu,” Bi Esther Musila aliandika kwenye Instagram.

Aliongeza, “Asante Mwenyezi kwa yote, kwa matukio ya ajabu na kwa kunifikisha hapa. Siichukulii kawaida. Umekuwa mwaminifu sana kwangu na ninakupa sifa zote. Hongera sana Esther.

Mumewe, Guardian Angel ni miongoni mwa Wakenya ambao wamejitokeza kumpongeza kwa hatua hiyo kubwa ya kikazi aliyopiga.

Katika ujumbe wake wa pongezi, mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alimtaja Bi Musila kuwa mpenzi wake na kubainisha kuwa yeye ni baraka kubwa.

“Hongera sana malkia wangu. Wewe ni baraka,” Guardian Angel alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na video nzuri ya mkewe akiimba pamoja na kucheza wimbo wake mpya ‘Moyo Wangu.’

Mwezi uliopita, Bi Musila aliwajibu wakosoaji wake ambao wamekuwa wakimkosoa kuhusu mpango wake wa kustaafu.

Katika taarifa, mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alibainisha kuwa watu kadhaa wamekuwa na maswali chungu nzima baada ya kuweka wazi kuwa ana mpango wa kustaafu katika shirika la UN katika miaka mitano ijayo baada ya kufanya kazi pale kwa zaidi ya miongo miwili.

Esther aliweka wazi kwamba bado ana takriban miaka 12 kabla ya kufikia umri wa kustaafu katika Umoja wa Mataifa lakini akadokeza kuwa hataki kusubiri ila badala yake anapanga kustaafu mapema.

”Kwa wale mnaouliza baada ya kuona mahojiano yangu, umri wa kustaafu katika UN ni miaka 65! Bado nina miaka 12 zaidi ya kufanya kazi nikitaka, lakini nina chaguo la kuondoka mapema..,” Esther alisema kupitia Instagram.

Aliongeza, “Heshimu uzee. Ni kesho yako ooo! Nina umri wa miaka 18 hadi nife.

Katika mahojiano na Standard Entertainment & Lifestyle, mke huyo wa  Guardian Angel alifichua kuwa anataka kustaafu hivi karibuni ili aanze kufurahia pesa zake kabla hajazeeka sana.

"UN imekuwa kazi yangu bora. Miaka 21 si muda mfupi, ni muda mrefu. Hivi karibuni ninatazamia kustaafu, labda katika miaka mitano ijayo. Nitakuwa nikistaafu, nataka kufurahia pesa zangu nikiwa bado mdogo,” Bi Omwaka alisema.

Aidha, alifichua kuwa amefanya kazi katika idara nyingi za UN kabla ya kufika katika idara ya Usimamizi wa Miradi ambako anafanya kazi kwa sasa.