"Huwezi kuwa DCI!" Size 8 azungumzia kwa nini hupaswi kugusa simu ya mpenzi wako

Size 8 ameolewa na DJ Mo kwa muongo mmoja uliopita na ndoa yao imekuwa na misukosuko mingi.

Muhtasari

•Size 8 alibainisha kuwa mpenzi ambaye amedhamiria sana kuenda nje ya ndoa atafanya hivyo bila kukamatwa licha ya kuchunguzwa.

•Size 8 aliwaomba wote walio kwenye ndoa kumuomba Mungu aziongoze ndoa zao na wenzi wao.

Size 8 na mume wake DJ Mo
Image: MpASHO

Mwimbaji  mashuhuri wa nyimbo za Injili wa Kenya, Linet Munyali, almaarufu Size 8 amewaonya watu walio katika ndoa dhidi ya kuchunguza simu za wapenzi wao.

Wakati akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, mke huyo wa mcheza santuri mashuhuri, Samuel Muraya almaarufu DJ Mo aliwataka wapenzi badala yake wamwamini Mungu kufichua uovu katika ndoa yao.

Alibainisha kuwa mpenzi ambaye amedhamiria sana kucheza karata nje ya ndoa atafanya hivyo bila kukamatwa licha ya kuchunguzwa.

“Wewe huwezi kuwa DCI. Ikiwa mtu anataka kufanya jambo fulani, atafanya tu. Kama mtu anataka kufanya kitu, atafanya rafiki yangu. Atakuwa na simu moja yenye anaacha kwa ofisi,” Size 8 alisema.

Aliongeza, “Jambo moja nililogundua kuhusu mtu, unapooana na mtu, alikuwepo hata kabla wewe haujakuwepo katika maisha yake. Wana mawazo yao wenyewe na ufahamu wao wa mambo yao wenyewe. Mtu anapotaka kunywa maji, iwe utamwambia anywe au la, atakunywa tu.”

Kufuatia hali hiyo, mama huyo wa watoto wawili aliwaomba wote walio kwenye ndoa kumuomba Mungu aziongoze ndoa zao na wenzi wao.

"Huwezi kumwamini mumeo 100%, na pia huwezi kumwamini mkeo 100%. Waachie mtu unayeweza kumwamini, Mungu,” alisema.

Size 8 amekuwa kwenye ndoa na mcheza santuri wa nyimbo za injili, DJ Mo kwa muongo mmoja uliopita na wawili hao wamejaliwa watoto wawili pamoja.

Mapema mwaka huu, mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alifichua kwamba huwa anaomba kabla ya wao kushiriki tendo la ndoa na mume wake DJ Mo..

Akizungumza kwenye chaneli ya YouTube ya Diana Chacha, alifichua kwamba huwa anaomba ili apate hamu ya kufanya mapenzi wakati  mumewe anapotaka lakini hajisikii tayari.

Pia alifichua kwamba kabla ya kuzamia kwenye mchezo huo wa kitandani, yeye kawaida humuombea mume wake DJ Mo apate nguvu za kumridhisha kama ambavyo angetaka.

"Akikuja huwa namshika nasema 'Baba katika jina la Yesu' (Huwa hajui). Huwa naambia Mungu ampatie nguvu nataka kujibamba," alisema.

Mhubiri huyo alibainisha kuwa huwa anafanya maombi hayo bila ya mumewe kujua.

"Huwa naomba kimoyomoyo namwambia Mungu ,' Mungu Baba patia huyu mwanaume nguvu, wewe ndiye uliumba tendo hili, Baba jinsi ulivyoliumba,nataka kulifurahia jinsi ambavyo uliona," alisema.

Size 8 aliweka wazi kwamba huwa anaomba mumewe aweze kumridhisha ili asiwahi kupatwa na fikra za kuenda nje ya ndoa.

DJ Mo kwa upande wake alisema wakati akielekea nyumbani, pia yeye hufanya ombi kwa Mungu akimsihi awape kipindi kizuri.

"Wakati akiomba na mimi nikiwa kwa gari huwa nasema atajua mimi ni nani," alisema.

Wanandoa hao waliwashauri wapenzi wengine kumshirikisha Mungu kila wakati wanaposhiriki tendo la ndoa.

"Watu hucheka wakiambiwa ati waombe kabla ya mapenzi. Yeye (DJ Mo) hajui, lakini mimi kwa upande wangu huomba," alisema