Juma Jux akiri kuumia sana moyoni wakati Vanessa Mdee alipotungwa mimba na Rotimi

"Niliumia. Sio mchezo niliumia kweli. Wakati huo niliumia sio mchezo,” Jux alikiri.

Muhtasari

•Jux amekiri kuwa alihuzunika sana alipopata taarifa kwamba Vanessa Mdee alikuwa akitarajia mtoto wake wa kwanza na Rotimi.

•Muda mfupi baada ya Vanessa Mdee kutangaza kuwa ni mjamzito zaidi ya miaka miwili iliyopita, Jux alitoa wimbo wa kumpongeza.

Image: INSTAGRAM// JUMA JUX

Mwimbaji maarufu wa Bongo R’n’B Juma Jux amekiri kuwa alihuzunika sana alipopata taarifa kwamba mpenzi wake wa zamani Vanessa Mdee alikuwa akitarajia mtoto wake wa kwanza na mpenzi wake wa sasa, Olurotimi Akinosho almaarufu Rotimi mnamo Septemba 2021.

Jux alikuwa akiimba wimbo wake wa ‘Sina Neno’ alioutoa zaidi ya miaka miwili iliyopita baada ya Vanessa kuzaa mtoto wake wa kwanza alipofunguka kuhusu jinsi jambo hilo lilimfanya ajisikie.

Baada ya kuimba maneno kadhaa ya wimbo huo, mashabiki waliokuwa wamejitokeza kumtazama akitumbuiza walimuuliza iwapo Vanessa kupata mtoto na mwanaume mwingine ilimuumiza na bila aibu akakiri kuwa aliumia sana.

"Niliumia. Sio mchezo niliumia kweli. Watoto wa hii town wana balaa kweli. Wakati huo niliumia sio mchezo,” Jux alisema.

Vanessa Mdee, ambaye alichumbiana na Jux kwa takriban miaka sita kabla ya kutengana naye mwaka 2019, alipata mtoto wake wa kwanza na muigizaji na mwimbaji wa Kimarekani mwenye asili ya Nigeria, Rotimi mwezi Septemba 2021 baada ya wawili hao kuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa takriban mwaka mmoja.

Muda mfupi baada ya Vanessa Mdee kutangaza kuwa ni mjamzito zaidi ya miaka miwili iliyopita, Jux alitoa wimbo wa kumpongeza.

Kwenye wimbo huo 'Sina Neno', Jux alimhakikishia Mdee kuwa hana ugomvi wowote naye kwani alishafunika yaliyopita kwenye kaburi la sahau.Alisema kuwa ana raha sana kuona  kuwa Mdee anafurahia ndoa yake ya sasa na muigizaji Rotimi na kumpongeza kwa kuwa alikuwa karibu kuitwa mama.

"Naona wameremeta, ngozi imenawili una furaha now,

Kitanda hakina siri, zao la tendo una kitumbo wow,

Mnapendeza sana na penzi liko kasi kasi

Mkipostiana, Instagram status..." Jux alisema kwenye wimbo huo.

Msanii huyo alisema kuwa hana chuki yoyote na Mdee na kudai kuwa anamwombea maisha ya furaha pamoja na mpenzi wake. Aliwashauri wawili hao wavumiliane na wasiwahi kugombana ili mtoto wao asiwahi pata shida.

"Najua una furaha kwa zawadi uliyopata.

Tena ulivyo shujaa,mtoto mama amepata. 

Na nyie msije gombana, mtoto asije akapata kash kash 

Uzuri kuvumiliana, matatizo mkadiscuss

Tulishafunika kurasa, mambo ya zamani yalishapita

Maisha mengine sasa, kuwa na amani hakuna vita

Sikuchukii nakuombea,

Maisha mema ya furaha, Mungu awaonyeshe njia

Siumii, nimezoea, ila nina furaha kuiona familia

Niko salama, Mimi sina neno" Jux aliimba.

Jux na Vanessa walitengana mwaka wa 2019 baada ya kuchumbiana kwa kipindi kirefu.