"Imeanza kunisumbua akili!" Eric Omondi azungumzia kuchukua kiti cha Jalang'o, Lang’ata

Eric alisema mahali imefika hana budi ila kufikiria kuwania kiti hicho kufuatia shinikizo kubwa lililowekwa juu yake.

Muhtasari

•Eric alifichua kuwa ameanza kufikiria kuwania kiti cha ubunge eneo la Lang’ata katika Kaunti ya Nairobi.

•Alidokeza kwamba yeye pamoja na viongozi wengine chipukizi wenye maslahi ya watu moyoni wanapanga kuwatimua wabunge wote waliokwenda kinyume na matakwa ya Wakenya.

wakati wa mkutano wa hivi majuzi na Raila Odinga.
Eric Omondi wakati wa mkutano wa hivi majuzi na Raila Odinga.
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji maarufu Eric Omondi amedokeza kuhusu mpango wake wa kujiunga na siasa na kuwania kiti cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika mazungumzo ya simu na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Eric alifichua kuwa ameanza kufikiria kuwania kiti cha ubunge eneo la Lang’ata katika Kaunti ya Nairobi.

Alisema kuwa wazo la kumridhi madaraka Jalang’o lilianza kumpata baada ya kusikia watu wengi wakimpendekezea awanie kiti hicho..

“Hii Lang’ata nimeiskia sana. Nikenda huko Naskia, nikienda huko naskia. Mimi mwenyewe nabaki nimepigwa na butwaa. Mimi mwenyewe naskia,” Eric alisema.

Aliongeza, “Sijasema natamani lakini naiskia. Sasa imeanza kunisumbua akili maanake nimeiskia sana. Mimi mwenyewe naskia na masikio yangu, ila sijasema na mdomo wangu."

Eric alisema mahali ilikofikia hana budi ila kufikiria kuwania kiti cha ubunge cha Lang’ata kufuatia shinikizo kubwa ambalo limewekwa juu yake.

“Lazima tuanze kufikiria maanake kuna vitu vingi. Tunapigwa teargas, tunaandamana, tunashikwa, tunafungwa lakini ikifika wakati wa kufanya maamuzi pale, wale wanasiasa wanapitisha Finance Bill wanaumiza Wakenya . Kisha wanaanchi wanamuita Erico aandamane lakini ikifika wakati wa kufanya maamuzi Erico hayuko huko ndani. Sasa inabaki ni kelele tu anapiga huko nje," alisema.

Mchekeshaji huyo alidokeza kwamba yeye pamoja na viongozi wengine chipukizi wenye maslahi ya watu moyoni wanapanga kuwatimua wabunge wote waliokwenda kinyume na matakwa ya Wakenya akitoa mifano ya zaidi ya wabunge 180 waliopigia kura kupitisha Mswada wa Fedha.

Katika miezi ya hivi majuzi, Eric amekuwa akijihusisha na mambo mengi yanayohusishwa na siasa, na hivyo kutoa dokezo kubwa kuwa anapania kujiunga na mchezo huo.

Mchekeshaji huyo hivi majuzi alikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga na mke wake Ida Odinga na kuzua uvumi kwamba anatayarisha njia yake ya kuwania kiti cha kisiasa. Kando na Raila na IDA, pia ameonekana akishiriki muda na viongozi wengine wa kisiasa nchini.

Eric pia amekuwa akijihusisha na shughuli zingine za hisani kama vile kuchangisha pesa mitandaoni katika juhudi za kuwasaidia Wakenya wenye mahitaji.  Hivi majuzi alishiriki kipindi cha moja kwa moja kwenye Instagram kwa saa nyingi katika harakati za kuchangisha pesa za kusaidia Wakenya walio na mahitaji.

Hatua za hivi majuzi za msanii huyo mwenye umri wa miaka 40 ni dalili tosha kwamba anajipanga kufanya jambo kubwa siku za usoni, jambo ambalo bado hajalitangaza wazi.