Jalang'o avunja kimya kuhusu maendeleo ya afya yake baada ya upasuaji wa mguu

Jalang'o alifanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kushoto mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya kupata jeraha mnamo Septemba 26.

Muhtasari

•Jalang'o alidokeza kuwa anakaribia kupona kabisa na akafichua kuwa ni wiki tatu tu zilizosalia kwake kuwa sawa kabisa.

•Baada ya kuruhusiwa kutoka, alifichua kuwa angesalia nyumbani ambapo angepitia safari yake ya wiki sita ya kupona.

Image: INSTAGRAM// JALANG'O

 Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o ametoa taarifa kuhusu maendeleo ya afya yake takriban mwezi mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu kufuatia jeraha.

Siku ya Alhamisi, mbunge huyo wa muhula wa kwanza alishiriki picha ya miguu yake ikionyesha mguu wa kushoto ukiwa na plasta ya kuusaidia katika mchakato wa uponyaji.

Kwenye maelezo ya picha hiyo, alidokeza kuwa anakaribia kupona kabisa na akafichua kuwa ni wiki tatu tu zilizosalia kwake kuwa sawa kabisa.

"Nakaribia kufika hapo.. Wiki 3 zimesalia!" Jalang’o alisema kupitia akaunti yake ya Instagram.

Mwanasiasa huyo wa ODM alifanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kushoto baada ya kuumia alipokuwa akifanya mazoezi na timu ya Bunge ya Mpira wa Kikapu mwishoni mwa mwezi uliopita.

Jalang'o aliruhusiwa kuenda nyumbani mwishoni mwa Septemba baada ya kulazwa katika Hospitali ya Nairobi kwa siku chache.

Baada ya kuruhusiwa kutoka, alifichua kuwa angesalia nyumbani ambapo angepitia safari yake ya wiki sita ya kupona.

"Ninataka kuchukua fursa hii kuwashukuru kila mtu kwa maombi yenu ya Kupona Haraka na ninyi nyote mlionitembelea katika Hospitali ya Nairobi," Jalang’o alisema kwenye Instagram mwishoni mwa mwezi jana.

Mwandani huyo wa rais William Ruto aliambatanisha taarifa yake na picha iliyomuonyesha akiwa amejipumzika kwenye sofa nyumbani kwake huku mikongojo ya kumsaidia kutembea ikiwa kando. Mguu wake wa kushoto ambao ulijeruhiwa ulikuwa umefungwa ili kumsaidia kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.

“Ninataka kushukuru timu nzima ya hospitali ya Nairobi inayoongozwa na Prof. Atinga kwa kazi nzuri na ukarimu wao wa jumla na huduma. Tuko chini lakini hatujatoka! Timu yetu ya Langata yenye uwezo itasimamia masuala ya eneo bunge yakifuatiliwa kwa karibu na mimi mwenyewe. ASANTENI saana!” alisema.

Akizungumzia jeraha lake, alifichua kuwa alipata ajali alipokuwa akifanya mazoezi na timu ya mpira wa vikapu ya Bunge mnamo Jumanne, Septemba 26.

Ajali hiyo ilimsababishia jeraha kubwa kwenye mguu wa kushoto na kupelekea yeye kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha sehemu iliyoharibiwa baada ya uchunguzi wa MRI.

"Jumanne iliyopita wakati wa mazoezi yetu ya asubuhi ya mpira wa kikapu ya Bunge nilipata ajali iliyorarua kano zangu, nilifanyiwa upasuaji wa kurekebisha na kurejea nyumbani wakati safari ya wiki 6 ya kupona inaanza," alisema.