Msanii

Msanii E-Sir alitabiri kifo chake.

Muhtasari

• Msanii Habib ambaye ni kakake marehemu E-SIR  Alhamisi ya tarehe 27/01/2022 amesema kwamba nduguye alitabiri kifo chake siku moja kabla ya mauko yake kumfika.

• Aidha ameongeza kwamba kifo cha ndugu yake kimemuadhiri kwa muda mrefu sasa, na akatoa shukurani zake kwa msanii Nameless ambaye amekuwa wa karibu na wa msaada mkubwa kwa familia yao tangu E-SIR atangulie mbele ya haki.

• Kwa upande wake Nameless amesema kwamba E-SIR ni mtu ambaye aliishi vizuri na watu na kujituma katika kazi zake

Msanii Habib ambaye ni kakake marehemu E-SIR  Alhamisi ya tarehe 27/01/2022 amesema kwamba nduguye alitabiri kifo chake siku moja kabla ya mauko yake kumfika.

Akizungumza na kituo kimoja cha habari, Habib alisema kwamba kabla ya kwenda kwenye hafla ya muziki iliyoandaliwa katika mji wa Nakuru, E-SIR alimwambia kwamba aliona maisha yake yakiwa yamefika mwisho na kumsihi kumshughulikia mama yao mzazi.

“Aliniuliza kati yake na mum nani napenda sana nikamwambia ni yeye, akaniambia basi wewe ni mjinga, mama ndo anakupenda zaidi,” alisema Habib.

Aidha ameongeza kwamba kifo cha ndugu yake kimemuathiri kwa muda mrefu sasa, na akatoa shukurani zake kwa msanii Nameless ambaye amekuwa wa karibu na wa msaada mkubwa kwa familia yao tangu E-SIR atangulie mbele ya haki.

Ikumbukwe kwamba E-SIR aliaga karibia  miaka kumi na tisa iliyopita wakati ambapo alikuwa kwenye kilele cha usanii wake.

Kipindi ambapo Mungu anaichukua roho yake, bingwa huyo alikuwa ametinga miaka ishirini na moja huku wengi wakisifia umahiri wake kwenye fani ya burudani licha ya umri wake mdogo. Alipoulizwa msukumo wake wa kuingia katika muziki, alisema anataka kukumbukwa daima.

Kwa upande wake Nameless amesema kwamba E-SIR ni mtu ambaye aliishi vizuri na watu na kujituma katika kazi zake na kwamba angebadilisha muziki wa taifa hili kabisa. Alisema kwamba E-SIR aliokoa maisha yake ila yeye akafariki , jambo ambalo anasema hajawahi kulielewa mpaka sasa.

Kwa mashabiki  wote na familia, ni ombi kwamba roho yake izidi kutulia penye wema.