Mwanawe Conjestina Achieng' asimulia jinsi ugonjwa wa akili wa mamake ulivyoanza

Muhtasari

•Chartone alisema bado haijawahi kubainika wazi kilichompelekea mama yake kukumbwa na matatizo ya kiakili.

•Ameeleza imani yake kuwa mama yake anaweza kuwa sawa tena huku akitoa wito kwa wasamaria wema kusaidia katika matibabu yake. 

Image: INSTAGRAM// CHARLTONE OTIENO

Charltone Otieno, mwanawe bingwa wa ndondi Conjestina Achieng' ameweka wazi kuwa mama yake bado anakumbwa na ugonjwa wa akili.

Bondia huyo chipukizi amefichua kuwa hali hiyo ilimpata mamake tena aliporejeshwa nyumbani kwao Nyanza baada ya kuwa rehab kwa miezi kadhaa.

"Alitoka hospitali akiwa sawa 70%, asilimia 30 iliyosalia ilipaswa kutatuliwa kama mipango ya baada ya matibabu. Mipango haikunda jinsi tulivyotarajia. Ilibidi Conje amerudi nyumbani. Cha kusikitisha ni kuwa akiwa pale nyumbani hana kazi na kutokana na hayo anaanza kufikiria mambo mengi, hali ambayo inasababisha msongo wa mawazo kisha ugonjwa unarudi," Charlton alisema katika mahojiano.

Chartone alisema bado haijawahi kubainika wazi kilichompelekea mama yake kukumbwa na matatizo ya kiakili.

Hata hivyo alitilia shaka madai kuwa hali hiyo ilichangiwa na mchezo wa ndondi huku akifichua kuwa mama yake alikumbwa na msongo wa mawazo kabla hajaugua.

"Nilikuwa hapo wakati ugonjwa huo ulianza. Tulikuwa kwa gym na yeye. Ghafla bin vu akaenda kwa corner ya gym akaanza kufikiria sana. Nilimuuliza ni nini akaniambia nitulie. Hiyo siku hakufanya mazoezi. Tulienda kwa nyumba jioni kama hajafanya chochote, akaenda akaoga akatulia kwa kiti. Asubuhi iliyofuata alikuwa amenyamaza. Ni kama alikuwa anazama kwenye msongo wa mawazo polepole bila sisi kugundua," Chartone alisimulia.

Alieleza kuwa hali ya mamake ilianza kukithiri hadi kufikia hatua ambapo alianza kugugumia maneno ambayo hayakueleweka.

Baadhi ya wanafamilia walisaidia kumpeleka bingwa huyo wa ndondi katika hospitali ya Mathare ambapo alihudumiwa.

"Mimi siwezi kujua ni nini ilitendeka. Pia watu hawaelewi. Lakini sio kwa sababu ya ndondi," Alisema.

Bondia huyo chipukizi ameeleza imani yake kuwa mama yake anaweza kuwa sawa tena huku akitoa wito kwa wasamaria wema kusaidia katika matibabu.