Fahamu ahadi za Wajackoyah kwa Wakenya iwapo atachaguliwa kuwa rais

Muhtasari

•Kura ya maoni ya hivi punde ya Radio Africa Group imeashiria kuwa umaarufu wake nchini umepanda kwa kiwango cha kugundulika.

•Wajackoyah ameahidi kutumia mapato ya uuzaji wa bangi na ukulima wa nyoka kulipa madeni yote ya Kenya kwa mataifa mengine.

Mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwa Lion's Place kwa mahojiano na Radio Jambo mnamo Juni 10, 2022.
Mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah akiwa Lion's Place kwa mahojiano na Radio Jambo mnamo Juni 10, 2022.
Image: CHARLENE MALWA

Profesa George Wajackoyah ni mmoja wa wagombea urais ambao waliidhinishwa ni IEBC kushiriki kinyang'anyiro hicho katika uchaguzi wa Agosti 9.

Wakili huyo anatazamia kumenyana na naibu rais William Ruto (Kenya Kwanza), Raila Odinga (Azimio- One Kenya) na David Mwaure (Agano).

Kura ya maoni ya hivi punde ya Radio Africa Group imeashiria kuwa umaarufu wake nchini umepanda kwa kiwango cha kugundulika katika kipindi siku za hivi majuzi.

Utafiti huo umeashiria kuwa Wajackoyah ndiye mgombea urais wa tatu kwa umaarufu huku akiungwa mkono na 2.7% ya waliohojiwa.

Hii ni ishara kuwa kuna asilimia fulani ya Wakenya ambao wanavutiwa na ahadi tatanishi ambazo amekuwa akitoa.

Katika makala haya tutaziangazia baadhi ya ahadi za Wajackoyah kwa Wakenya:-

Uhalalalishaji wa Bangi: Mgombea urais huyo wa Roots Party ameahidi kuhalalisha ukulima wa bangi na matumizi yake kwa minajili ya matibabu.

Akizungumza baada ya kuidhinishwa kuwania urais siku kadhaa zilizopiata, Wajackoyah alisema anatazamia kufanya maeneo ya  Bunyore, Mlima Kenya, Nyamira na Kisii kuwa maeneo makuu ya kilimo cha mmea huo ambao kwa sasa ni haramu hapa nchini.

"Bunyore katika mkoa wa Nyanza kuna mojawapo ya hali bora ya anga  ya kukuza bangi kwa sababu inakua kiasili. Nyamira Kisii na eneo la Mlima Kenya zitakuwa kipaumbele chetu kwa sababu tunataku kuinua Bunyore kuwa kaunti na huenda tutakuwa tunaagiza wakazi wa Bunyore kuwa na  bangi zao kuu," Alisema Wajackoyah.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na runinga ya Citizen, Wajackoyah alidai kuwa Wakenya wataruhusiwa kulima bangi kwa ajili ya kuuza nje, hatua ambayo anasema itaongeza mzunguko wa pesa katika uchumi huku akidai kuwa gunia moja linaweza kuuzwa kwa dola milioni 3.2.

Ukulima wa nyoka: Hivi majuzi  Wajackoyah sasa alieleza kuwa ufugaji wa nyoka pia utakuwa mojawapo ya mikakati yake wa kuongeza mapato ya serikali na kulipa madeni ya nchi kwa mataifa mengine.

Akiwa kwenye mahojiano na Citizen, mgombea urais huyo alisema ufugaji wa nyoka ni mradi wa faida ambao serikali yake itazingatia iwapo atachaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9.

"Tunaanzisha ufugaji wa nyoka nchini ili tuweze kukamua sumu ya nyoka kwa madhumuni ya dawa, watu wengi wanaumwa na nyoka hapa nchini na inabidi msubiri dozi kutoka nje ya nchi kupitia shirikisho la dawa," Wajackoya alisema.

Alisema baada ya utoaji wa sumu nyoka hao watasafirishwa nje ya nchi kama chakula kwa nchi zinazokula nyama yake.

Adhabu ya kifo kwa wafisadi: Wajackoyah ameapa kuwa viongozi wafisadi hawatapata nafasi katika serikali yake.

Mara nyingi amenukuliwa akisema ataweka adhabu ya kifo kwa wale wote wanaoshiriki ufisadi na ubadhirifu wa pesa na mali za umma.

“Adhabu ya kifo ndio njia pekee. Katika miaka mitano ya kwanza ya uongozi wangu, nitahakikisha hawa wabadhirifu wote wamehisi uchungu na ugumu wa maisha ambao wamewasababishia Wakenya ufujaji na wizi wa mali ya umma bila huruma,” Wajackoyah aliwahi kusema katika mahojiano na KTN.

Wajackoyah anasema hatua hiyo itamuwezesha kugeuza hali ya uchumi wa nchi na kukabiliana na ufisadi.

Kutupilia mbali katiba: Wajackoyah ameahidi kuwa ataisimamisha Katiba ya Kenya na kutumia utawala wa udikteta kwa muda wa miezi sita ikiwa  atachaguliwa.

“Tutasimamisha katiba kwa sababu ina kanuni na taratibu zisizo za lazima,” alisema katika mahojiano na Citizen.

Kulipa madeni ya nchi: Mgombea urais huyo wa Roots Party ameahidi kutumia mapato ya uuzaji wa bangi na ukulima wa nyoka kulipa madeni yote ya Kenya kwa mataifa mengine.

Wajackoyah amesema mapato yatakayokusanywa kutokana na ukulima wa bangi  yataiwezesha nchi kulipa madeni ambayo inadaiwa huku akidai kuwa gunia moja linaweza kuuzwa kwa dola milioni 3.2.

"Suluhu ya deni la taifa ni kukuza bangi ambayo itaiwezesha nchi hii kulipa deni lote lililobaki," alisema katika mahojiano na Citizen.

Kuhamisha mji mkuu: Mgombea urais huyo pia ameahidi kuhamisha jiji kuu kutoka Nairobi hadi eneo la North Eastern.

Alisema kuhamisha mji mkuu kutalifungua eneo la North Eastern kama mji mkuu wa utawala na kuiruhusu Nairobi kuwa eneo kuu la viwanda.