Bahati: Sijawahi shikwa nikicheat, Diana ana password zangu, sina password zake

Bahati alisema kwamba mwaka wa kwanza katika ndoa Diana alitoroka nyumbani mara tatu.

Muhtasari

• "Kitu kimoja ambacho alikuwa anateta sana mpaka kuondoka nyumbani ni wakati wangu kwake" - Bahati

• Msanii huyo alisema licha ya wao kuweka wazi mapenzi yao kwenye mitandao, lakini pia hupitia changamoto za kindoa kama ndoa nyingine.

Bahati na mkewe Diana Marua
Image: Diana Marua (Istagram)

Kwa mara ya kwanza katika safari ya muziki wa Diana B, Mumewe Bahati amezungumzia kwa upana zaidi nini kilichomvutia mkewe kujitosa katika Sanaa hiyo na ni kwa nini huwa mashabiki wake hawamsikii sana akiachia madude ya kufoka kama alivyojitambulisha katika ngoma zake za kwanza mbili.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo kimoja cha redio nchini, Bahati alisema kwamba mkewe kuingia kwenye muziki halikuwa jambo la kuhamia kabisa kwenye kitivo hicho bali tu ni kujifurahisha kwani muziki wa rap anaufanya kama njia moja ya kujiburudisha.

Alifichua kwamba Diana Marua amewekeza nguvu na muda wake mwingi kwenye kukuza maudhui mtandoni YouTube na suala la mziki ni kama kiki ya pembeni tu kujiburudisha, akini akapata mashabiki wake wamempa mapokezi makubwa kimuziki.

“Yeye si mtu wa kupenda kuimba sana, ana sehemu yake anaipenda ambayo ni kukuza maudhui YouTube na mimi niliona nimuache tu afanye hivyo,” alieleza Bahati.

Pia alifichua kwamba Diana B hujiandikia mwenyewe mashairi yake ya kutema madini kwa mtindo wa kufoka.

Akiulizwa iwapo ndoa yao imewahi pata changamoto, Bahati alisema kwamba licha ya kuwa wanayaonesha mahusiano yao wazi kwenye mitandao ya kijamii, bado huwa na changamoto na hadi kukumbuka kwamba Diana Marua aliwahi kuondoka nyumbani katika mwaka wao wa kwanza.

“Wakati tunaanza kuchumbiana, kawaida tu uchumba na ndoa yoyote, tulikuwa na changamoto kibao haswa mwaka wa kwqanza aliwahi ondoka nyumbani tena mara kadhaa. Aliondoka nyumbani kama mara mbili tatu hivi na kwa mwaka hiyo ni mara kadhaa. Kitu kimoja ambacho alikuwa anateta sana mpaka kuondoka nyumbani ni wakati wangu kwake kwa sababu kipindi kile nilikuwa nashinda sana kwa studio nikisimamia rekodi lebo yangu,” alisema Bahati.

Mtangazaji alipotaka kubaini zaidi sababu zingine za kumfanya mkewe kuondoka nyumbani kipindi hicho, msanii Bahati alisema kwamba kikubwa zaidi ni hilo la muda na kusema pia wakati huo mkewe alikuwa na mtoto mchanga. Alikana kabisa madai kwamba mkewe pengine alipata ujumbe wa mapenzi katika simu yake na ndio sababu mojawapo ya kuondoka nyumbani.

“Sijui kama hii ndio njia nzuri ya kujibu hilo lakini acha niseme sijawahi shikwa. Sijawahi fumaniwa. Yeye ana nywila za simu zangu zote ila mimi sina zake kwa sababu huwa tu sitaki,” alisema Bahati.