Oti wa filamu ya Nairobi Half Life azirai na kuaga dunia

Muigizaji huyo alishinda tuzo ya muigizaji bora mwaka 2016.

Muhtasari

• Miana Wilfred Olwenya alifahamika na wengi kwa jina la Oti alilolitumika katika filamu ya Nairobi Half Life.

Muigizaji wa Nairobi Half Life
Maina Wilfred Olwenya Muigizaji wa Nairobi Half Life
Image: Instagram

Muigizaji maarufu nchini Kenya Maina Wilfred Olwenya, anayefahamika zaidi na wengi kutokana na weledi wake katika filamu iliyoshinda tuzo nyingi nchini ya Nairobi Half Life, amefariki dunia.

Olwenya ambaye alivaa magwanda ya jina Oti katika filamu hiyo maarufu anasemekana kuzirai Jumatatu jioni na alipokimbizwa hospitalini madaktari walitangaza kifo chake.

Wengi wamemuomboleza muigizaji huyo nguli na kumtaja kuwa kigezo kikubwa katika mafanikio makubwa katika mauzo ya filamu ya Nairobi Half Life.

Oti, kama alivyokuwa akifahamika na wengi alikuwa anaigiza katika filamu hiyo kama jambazi mmoja ambaye alikuwa na uswahiba wa kushikwa mara kwa mara na kupelekwa rumande na kisha kuruhusiwa kutoka baadaye.

Aliigiza kama kiongozi wa kundi fulani la kihuni jijini Nairobi ambalo lilikuwa likiwahangaisha watu kwa kuwaibia vitu vidog vidogo kama simu na kubomoa sehemu za magari ya wenyewe na kuziuza kaam bidhaa kuukuu.

Oti alikuwa ni mtu mwenye urafiki wa siri na vyombo vya dola ambapo kila baada ya kuibia watu alikuwa anatoa hongo wa polisi ili kufumbia macho uhuni wake na kundi lake.

Filamu hiyo inaisha pale ambapo Oti na kundi lake wanashindwa kuelewana na kundi lingine la Rafiki yake kwa jina Dingo ambapo wanaanza vita vikali kutokana na mzozo wa kugawana pesa walizozizoa kutokana na mauzo ya gari la waliloliiba, na makundi yote mawili yanapigana kabla ya polisi kuingilia kati na kuwakamata wahuni hao wote, Dingo anafariki baada ya kuangushiwa kiziki na muigizaji mmoja kwa jina Mwas kwenye filamu hiyo.

Kundi la Oti linatengwa na kupelekwa katika makaazi mahame ambapo polisi wanaanza kuwaua mmoja baada ya mwingine, Oti wanajaribu kutibua njama ya polisi kuwaua lakini juhudi zao zinagonga mwamba pale anapojaribu kutorokea dirishani lakini kwa bahati mbaya anapatwa na risasi moja ya moto mgongoni.

Kutokana na jinsi alivyovaa igizo hilo kama Oti, msanii Olwenya alishabikiwa na wengi na mwaka wa 2016 alitajwa kuwa muigizaji bora nchini Kenya na kutuzwa.

Buriani Olwenya!