Mchekeshaji wa Churchill Show, Nasra Yusuf apoteza ujauzito wake

Mchekeshaji huyo aliomboleza kupitia Instagram yake akisema kutomuona mwanawe kumemvunja moyo sana.

Muhtasari

• Mchekeshaji huyo hata hivo alimsifia mumewe kwa kusimama naye imara kumfariji hata kama yeye pia alihitaji kufarijiwa.

Mchekeshaji wa Churchill Show
Nusra Yusuf Mchekeshaji wa Churchill Show
Image: Instagram

Mchekeshaji wa Churchill Show, Nasra Yusuf na mumewe Rashidi wametangaza habari za tanzia Jumatatu adhuhuri ambapo wameweka wazi kwamba wanao waliyekuwa wakimtarajia amefariki kabla ya kuzaliwa.

Akipasua mbarika ya habari hizo za kuhuzunisha, mchekeshaji Nasra Yusuf alisema kwamba hii imekuwa moja kati ya siku mbaya zenye simanzi kubwa katika maisha yake ya ukubwani.

Mchekeshaji huyo pia aliandika kwamba amepoteza zawadi yake kabla hata ya kuipokea mikononi licha ya kuweka maandalizi mazuri kutoka jina, nguo na kila kitu kinachohitajika katika maandalizi ya kumpokea mtoto anapozaliwa.

“Kumpoteza malaika wangu mdogo kabla hata sijakutana naye hufanya iwe vigumu zaidi kuamini 💔💔Nilifurahia sana safari hii, nilikuwa na kila kitu, kuanzia jina, hadi aina ya maisha ambayo angefikiria akilini mwangu..ooh natamani kuuona uso wako tu mtoto wangu💙💓lakini ALHAMDHULILAH,” Nasra Yusuf aliomboleza.

Yusuf aliombolexa kifo cha kijusi chake na kusema kwamba haamini amefariki lakini pia akashukuru kwa kusema kuwa huenda huyo ndiye atakayekuwa bahati yake ya kuingia peponi.

Katika hali ya kujipa tumaini, Yusuf alisema kwamba alifurahia kwamba aliishi na ujauzito huo hadi kuifahamisha familia, ndugu , jamaa na marafiki kuhusu ujio wake, japo safari hajaikamilisha kama walivyotarajia wengi kumuona.

“Kwa kweli nimefurahi sana kwamba tulipata kushiriki habari za ujio wako na familia yetu, marafiki na mashabiki ambao wote walikupenda, natumai umehisi upendo kutoka kwetu sote mtoto,” Nasra Yusuf alijitia moyo.

Kwa uchungu mkubwa, mchekeshaji huyo alikubali kwamba hatoweza tena kumuona mwanae kwa kujiliwaza kwa maneno kwamba yakishamwagika hayazoleki. Pia amemlimbikizia sifa mumewe muongozaji wa filamu, Rashid na kusema kwamba amesimama naye bila kutetereka haswa katika wakati huu mgumu wa mama kumpoteza mwanae hata kabla ya kumpakata.

“Mwanaume wangu alikuwa amevunjika moyo, sikuwahi kumuona akiwa na huzuni kiasi hicho, lakini bado, alichagua kuwa imara kwa ajili yangu, akinifariji wakati yeye pia alihitaji kufarijiwa na kwenda juu zaidi ili kuhakikisha kwamba ninapata matibabu bora zaidi.. yale maneno yake kuwa "babe Niko hapa, tutatembea hii safari pamoja na tutakuwa sawa pamoja” yalikuwa na maana kubwa sana kwangu,” aliomboleza mchekeshaji huyo.