Diamond ailaumu 'media' ya Tz kumchonganisha na Alikiba, "Wanapenda mwanamuziki afe" (video)

Alisema vyombo vya habari vya Tanzania ndivyo vilivyounda dhana ya ugomvi baina yake na Alikiba

Muhtasari

• Diamond alisema yeye hana ugomvi wowote na Alikiba na wala hawajawahi kugombana hata siku moja.

• Pia alisema endapo Kiba atamuita kufanya collabo bila chuki yeye atajitokeza na kushiriki.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na minong’ono mitandaoni na hata kwenye vyombo vya habari kuhusu ugomvi na uhasama kati ya masupastaa wawili wa muziki wa Afrika Mashariki, Diamond Platnumz na Ali Kiba.

Katika mahojiano ambayo yamepakiwa kwenye mtandao wa YouTube juzi kati na mtangazaji Mzazi Willy Tuva wa humu nchini, Diamond anasikika akieleza be na te kuhusu suala hilo zima la uwepo wa ugomvi kati yake na Alikiba.

Diamond anaanza kwa kuweka wazi kabisa kwamba yeye na Alikiba wala hawajawahi kugombana na kuwa na ugomvi wa aina yeyote na kulaumu uvumi huo kwa vyombo vya habari vya Tanzania ambavyo kulingana na yeye ndivyo vinajaribu kuunga dhana kwamba kuna uhasama baina ya wasanii na watu wanapolikumbatia hilo basi habari hiyo huenea na kufasiriwa kama kweli.

Platnumz alisema kwamab tatizo la watu wengi ni kujaribu kulinganisha kazi za msanii mmoja na mwingine na hapo ndio tatizo huanzia.

“Watanzania wanapenda mwanamuziki afe, yaani akipanda ashuke. Wakiona msanii anafanya vizuri, wanajaribu kumchonganisha naye wakipitia yule msaani mwingine, ambayo mimi naona sio vizuri. Kitu ambacho kilinisikitisha sana ni kwa nini watu watengeneze hasa vyombo vya habari kutoka nyumbani Tanzania kuonyesha mimi nina tatizo na Ali Kiba. Mimi sina tatizo na Ali. Sijai gombana naye kabisa," alisema Diamond Platnumz.

Vile vile simba huyo wa Bongo Fleva alisema kwamba ni kawaida ukiwa mtu maarufu si kila mtu atakukubali na kukupenda kwani hata wale wanaojisogeza karibu na wewe utakuja kugundua ni maadui wako wakubwa wanaokukandia chini kwa chini ili ufeli ndio washangilie.

Alisema kwamba msanii ukikubali kubebwa na wimbi hilo kutoka baadhi ya watu basi jua fika utakosana na kila mtu.

“Ukiwa msanii hana akili, utagombana na kila mtu, lakini mimi naelewa vyombo vya habari na baadhi ya mameneja wanafanya kazi na wasanii wao, wanafikiri ukimchonganisha mtu na msanii ndio unampandisha kumbe mwanzo unaua soko la nyumbani,” Diamond Platnumz alifunguka.

Diamond alipuuzilia mbali uhasama kati yake na Alikiba na kusema kwamba ikiwa Kiba atamuita kwa collabo bila shaka yeye atajitokeza na kushiriki.