Wahu afurahia kutarajia mtoto wa 3 na miaka 17 katika ndoa na Nameless

Wahu alisema kuwa anashukuru kumtarajia mtoto wao wa tatu

Muhtasari

• Mume wake Wahu, Nameless pia alipakia picha hizo katika ukurasa wake wa Instagram, pia yeye akiwa mwenye furaha kwa hatua hiyo mpya ya maisha yao.

• Hivi majuzi walionyesha mtandaoni kuwa walikuwa wanajitayarisha kumpokea mtoto wao mtarajiwa na walivyokuwa na furaha na bashasha kama familia.

Wahu// Nameless

Mwanamuziki Wahu ameweka katika ukurasa wake wa Instagram picha aliopiga akiwa na mumewe Nameless kuonyesha kumbukumbu za ujauzito wake.

Wahu aliiweka picha hiyo iliyoonyesha wawili hao kuwa na hamu ya kutarajia mtoto wao wa tatu.

Katika picha hiyo aliyochapisha mtandaoni, Wahu alisema kuwa anashukuru kumtarajia mtoto wa tatu na kwa yote ambayo yamekuwa yakiendelea.

"Siwezi chukulia kitu chochote poa," Wahu alisema huku akiwa amekumbatia tumbo lake.

Mumewe Wahu, Nameless vile vile alipakia picha hizo katika ukurasa wake wa Instagram, akiwa mwenye furaha kwa hatua hiyo mpya ya maisha yao.

Alisema kuwa anamshukuru Mungu kwa hatua hiyo mpya na kwa kuwawezesha kufika walipo sasa baada ya kuwa pamoja kwa miaka 17.

“Familia ya Mathenge, ahsante Mungu kwa kutufikisha hatua hii katika maisha yetu,” Nameless aliandika huku akiwa amemkumbatia mkewe Wahu kwa mahaba.

Wanamuziki hao bado hawajafichua jinsia ya mtoto wanaomtarajia hata baada ya mashabiki wao kuwauliza kuhusu kuandaa sherehe ya kufichua jinsia ya mtoto wao mtarajiwa.

Hivi majuzi walionyesha mtandaoni kuwa walikuwa wanajitayarisha kumpokea mtoto na walikuwa na furaha kama familia.

Walikuwa wakifanya maandalizi hayo kwa kununua nguo na vitu vingine vya mtoto ingawa mama huyo alisema kuwa wamefanya matayarisho hayo kwa dakika za mwisho kabla kujifungua.

Alisema kwamba kutokuwa kwenye hali hiyo kwa muda mrefu kumemfanya aanze upya kununua bidhaa za mtoto kwa sababu watoto wao wawili ni wakubwa sasa.

Nameless na Wahu walisherehekea miaka 17 ya ndoa yao, walifunga pingu za maisha mwaka wa 2005 na wamebarikiwa na watoto wawili.

Wamekuwa wakishirikiana kwenye taaluma yao ya muziki na hata kutoa nyimbo pamoja kama ilivyokuwa enzi ya zamani.