Fahamu wanawake wa injili waliovunja ndoa zao za kwanza na kuolewa tena

Wikendi iliyopita, Gloria Muliro alikuwa anasherehekea mwaka mmoja katika ndoa ya pili baada ya kuvunja ndoa yake ya kwanza iliyodumu miaka 6.

Muhtasari

• Orodha hii ni ya wanawake wa Kenya ambao wanahubiri injili na ambao waliwahi kuvunja ndoa zao za kwanza na kuingia ndoa za pili.

Baadhi ya wanawake wainjilsti walivunja mahusiano yao na kuolewa tena
Baadhi ya wanawake wainjilsti walivunja mahusiano yao na kuolewa tena
Image: Instagram

Wikendi iliyopita mwinjilisti wa muda mrefu Gloria Muliro alikuwa anasherehekea mwaka mmoja tangu kufunga ndoa yake ya pili na mchungaji Evans Sabwami.

Kumekuwepo dhana ambayo inawazungumza watu wanaohubiri injili kuwa hawafai kuvunja ndoa zao na kuingia katika ndoa nyingine katika kile wengi wanahoji kwamba ni kinyume na matakwa ya Mungu yule wanayemhubiri.

Katika Makala haya, Radiojambo.co.ke inakuandalia orodha ya watumishi wa Mungu wa kike ambao walivunja ndoa zao za kwanza na kuingia katika uhusiano wa pili wa kimapenzi.

Gloria Muliro na Mchungaji Omba

Muliro na Mchungaji Omba walikuwa katika ndoa kwa miaka 6 baada ya mwimbaji huyo kusema imetosha na kuivunjilia mbali ndoa yake.

Alimshtumu mchungaji Omba kwa kumnyanyasa na pia matumizi mabaya ya pesa zake amabzo alikuwa anazipata kutokana na kazi zake za muziki wa injili.

Mwaka jana, Muliro na mchungaji Evans Sabwami walifunga ndoa ya kifahari iliyohudhuriwa na watu wachache huko New York Marekani baada ya kuandaa hafla ya matayarisho jijini Eldoret, Kenya wiki moja kabla.

Betty Bayo na Mchungaji Victor Kanyari

Betty aliolewa na Mchungaji Victor Kanyari, na baada ya kufichuliwa kwa mchungaji huyo jambo ambalo liliharibu ndoa yao, alipoteza imani na baba wa watoto wake wawili.

Ufichuaji wa panda mbegu ya 310 ulimfanya Betty kukimbilia Marekani na watoto wake na baadaye walitengana aliporudi.

Mwaka jana, mkali huyo wa ‘Elevent Hour’ alifunga ndoa tena na mpenzi wake Hilam Gitau baada ya kuchumbiana kwa miaka 2.

Nicah the Queen na Dr Ofweneke

Nicah aliolewa na mchekeshaji Dr. Ofweneke na walijaliwa watoto 2 lakini ndoa iligonga mwamba Nicah alipomtuhumu Ofweneke kwa kumpiga na kumnyanyasa. Alikuja kwenye mitandao ya kijamii na picha kuthibitisha tuhuma hizo na kusababisha kuachana kwao.

Baada ya miaka kadhaa ya kutengana, Nicah alidhibitisha kwamba amempata mume mwingine ambaye ni mcheza santuri DJ Slahver.

Eunice Njeri na rapa Izzo

Njeri aliwashangaza wengi baada ya kuvunja uhusiano wake na rapa huyo kutoka Uganda, takriban miezi miwili tu baada ya kufunga pingu za maisha.

Wawili hao walifanya harusi yao nchini Marekani lakini baadae Njeri alivunja ndoa hiyo na kurudi nchini Kenya baada ya kudai kwamba alikuwa anahisi kukosa nyumbani kwao – Afrika.

Miezi miwili iliyopita, Njeri aliweka wazi kwamba amekuwa katika uhusiano mwingine na hata kujaaliwa mtoto na mpenzi wake wa pili.

Alisema kwamba mume wake mpya, aliyemtambulisha kwa jina moja kama Muthii walikutana 2019, wakaoana 2021 na mwaka huu Agosti walijaaliwa na mtoto wa kiume.

Keziah Kariuki na Muthee Kiengei

Muthee Kiengei alibwawa na aliyekuwa mwanahabari wa runinga ya Kameme Keziah Kariuki katika kile Keziah alisema alivunjika moyo baada ya Kiengei kuoa mke wa pili.

Baada ya kumuacha Kiengei, Keziah alifunga ndoa na mfanyibiashara George Njoroge mwishoni mwa mwaka jana.

Kariuki na Kiengei wakati wa ndoa yao, walijaaliwa na binti mmoja ambaye sasa ana takriban miaka 8.