Mwanaume kamili humbebea mkewe mkoba na kumpikia - Terence Creative

Alionekana kutilia kwenye mizani gumzo la mume wa gavana Kawira kumbebea mkoba wake.

Muhtasari

• Mkewe Milly Chebby alimshukuru kwa kumuonesha mapenzi si tu faraghani bali pia hadharani.

Terence creative na mkewe
Terence creative na mkewe
Image: Instagram//Terence Creative

Mwigizaji Terence Creative ameonekana kuingilia kati gumzo linalozidi kupenya kwenye mitandao ya kijamii baada ya mumewe gavana wa Meru Kawira Mwangaza kuonekana akiwa abembebea mkoba wake wa mkononi.

Murega Baichu alionekana katika moja ya picha zilizosambazwa mitandaoni akiwa na mkoba wa mke wake na kuzua mjadala mkali baina ya makundi mawili, baadhi wakidai kwamba mwanaume hafai kumbebea mkewe mkoba huku wengine wakisema kwamba kumbebea mkeo mkoba ni ishara ya kuonesha upendo na kumthamini mpenzi wako.

Terence alipakia picha akiwa pamoja na mkewe nje ya nyumba huku ameubeba mkoba wake na kufunguka kwamba wanaume wa kweli aghalabu huwasaidia wake zao kubeba mikoba yao pasi na kutiwa kiwewe na kile ambacho jamii inasema.

“Wanaume halisi huwabebea wake zao mikoba, kuwapikia chamcha, kuwafungulia mlango, kuwavutia kiti ili wakae miongoni mwa vitendo vingine vya kimahaba. Tuko pamoja kweli,” Terence aliandika.

Mkewe Milly Chebby alimsifia pakubwa kwa kauli hiyo huku akitaka maneno hayo ambayo aliyataja kama ushauri kuwafikia wanaume wenye misimamo cha kizamani kuwa mwanaume kumbebea mkewe mkoba ni kukaliwa katika ndoa.

“Ifikie bestie tafadhali asante babe kwa kuwa huna aibu ya kunipenda faragha na hadharani,” Milly Chebby alisema.

Terence na mkewe miezi michache iliyopita walisherehekea kufikisha miaka 10 katika ndoa kwa kukumbushana jinsi maisha yao yalianza kwa hatua za chini ambapo alidokeza kuwa walikuwa wanaishi kihayawinde sana.

Alipata upenyo kwenye sinia la utajiri mapema mwaka jana alipofanya filamu ya kuigiza kama mwanaume wa Kikongo mwenye pesa nyingi.