Nilikaa mlimani kwa siku 21 bila kula, maombi tu! - Christina Shusho

Alisema kwamba kwa sasa amemaliza miaka 3 tangu afungue kanisa lake na anafurahia watu kumuita mchungaji au kwa jina lake halisi.

Muhtasari

• Nilikuwa napanda ndege kwenda Kenya mlimani kuomba kule kuna vituo vya maombi vingi vizuri, nilikaa huko siku 21 bila kula chakula - Shusho.

Christina Shusho
Christina Shusho
Image: Instagram

Mwanamuziki wa nyimbo za injili kutoka Tanzania Christina Shusho ameibuka na madai kwamba aliwahi kaa mlimani kwa wiki tatu yaani siku 21 bila kula kitu chochote.

Alisema kuwa aliamua kuchukua uamuzi huo wa kuenda mlimani baada ya kuhisi msukumo fulani kutoka ndani mwake uliomtaka kukwea mlimani kwa ajili ya maombi.

Alisema kwamab hangeweza kulifanya jambo hilo Tanzania na hivyo aliabiri ndege kuja Kenya kwa kile aliitaja kuwa humu kuna vituo vya kufanya maombi vingi tena vizuri tu milimani ambako alifanikisha kufanya maombi kwa siku 21 pasi na kula bali maombi tu usiku na mchana.

Nilikuwa nasikia kitu ndani yangu natakiwa kukifanya. Nilikuwa napanda ndege kwenda Kenya mlimani kuomba kule kuna vituo vya maombi vingi vizuri, nilikaa huko siku 21 bila kula chakula,” Shusho alinukuliwa na vyombo vya habari Tanzania.

Alisema kwamba baadae aliporudi Manseze nchini Tanzania, alijiwa na msukumo mwingine uliomtaka kuanza kuhubiri kama vile Jonah wa Biblia.

Alilazimika kuanza kuhubiri hata kama muda huo hakuwa anajua kuhubiri kabisa lakini ilimbidi kwa sababu alikuwa ameingiwa na upako na uwepo wa Mungu.

“Nikaanza kufunguka picha kidogo kidogo, siku ya kwanza kuwaita watu Manzese pale tulikula nyama choma na ndizi hakukuwa na maombi. Baada ya hapo picha ikaanza kubadirika kwamba nafaa tu kuwa hapo. Nilianza kuhubiri pale kwa mara ya kwanza na nilikuwa sijui kuhubiri. Nilianza kuhubiri na mapepo yalianguka, nimefungua kanisa sasa ni miaka mitatu, mnaweza kuniita vyovyote iwe Mchungaji au Christina Shusho.”